Bodi ya Wadhamini wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) imewasilisha barua kwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania ikimtaka Jaji Hamidu Mwanga kujiondoa kusikiliza kesi ya madai iliyofunguliwa na baadhi ya wajumbe wa zamani wa chama hicho kutoka Zanzibar.
Wajumbe hao ni Said Issa Mohamed, aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis (Makamu Mwenyekiti Mstaafu), na Maulida Anna Komu, ambao wanajitambulisha kama wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa chama hicho kutokea Zanzibar.
Uamuzi na amri zilizotolewa na Mahakama mnamo Juni 10, 2025, ndizo zilizowasukuma wadaiwa kuandika na kuwasilisha barua ya kumkataa Jaji Mwanga kwa madai kuwa kwa mwenendo wa awali wa shauri hilo, hawana imani naye kuwa ataweza kuwapatia haki. Sambamba na barua hiyo, Bodi ya Wadhamini pia iliwasilisha maombi ya kuondoa amri hizo za Mahakama.
Wakati kesi hiyo ilipoitwa leo, Alhamisi Julai 10, 2025, kwa ajili ya kuanza kusikilizwa mbele ya Jaji Mwanga, Mahakama iliielezwa kuwa jaji hayupo kutokana na majukumu mengine katika Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, na hivyo kesi ikaahirishwa mbele ya Msajili Aziza Mbage hadi Julai 14, 2025.
Kiongozi wa jopo la mawakili wa wadaiwa, Wakili Mpale Mpoki, aliieleza Mahakama kuwa Bodi ya Wadhamini iliwasilisha barua ya kumtaka Jaji Hamidu Mwanga ajiondoe katika usikilizwaji wa shauri hilo.
"Wanaomba na kumtaka Jaji Hamidu Mwanga ajitoe katika usikilizwaji wa shauri hili. Pia tulileta shauri la maombi ya kuondoa amri za Mahakama hii zilizotolewa Juni 10, 2025, katika shauri namba 8960/2025, ambalo tayari limeshasajiliwa," alisema Wakili Mpoki.
Barua hiyo iliandikwa tarehe 23 Juni 2025 na kuwasilishwa kwa Naibu Msajili Juni 24, 2025.
Kutokana na kuwepo kwa maombi hayo, kesi ya msingi imesimama kwa muda usiojulikana hadi pale Mahakama itakapotoa uamuzi kuhusu maombi ya kumwondoa Jaji na ya kuondoa amri zilizotolewa awali.
Katika kesi hiyo ya madai, walalamikaji wanadai kuwa CHADEMA imekuwa ikiitenga Zanzibar katika uendeshaji wa shughuli za chama, hasa katika mgawanyo wa rasilimali za fedha na mali.
"Kuna mgawanyo usio wa haki wa mali za chama kati ya Tanzania Bara na Zanzibar," wamesema walalamikaji katika hati yao ya madai.
Pia wanadai kuwepo kwa vitendo vya ubaguzi wa kidini na kijinsia, pamoja na matamko yenye nia ya kuvuruga Muungano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa msingi huo, wanaiomba Mahakama Kuu:
-
Itamke kuwa wadaiwa wamekiuka kifungu cha 6A(1), (2), (5) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 Marejeo ya mwaka 2019;
-
Itamke kuwa ugawaji wa fedha, mali na rasilimali unaofanywa na wadaiwa kati ya Tanzania Bara na Zanzibar ni kinyume cha sheria na batili;
-
Iamuru kusitishwa kwa muda kwa shughuli zote za kisiasa hadi kutakapokuwepo na utekelezaji wa maagizo ya Mahakama;
-
Itoe amri ya zuio la kudumu dhidi ya matumizi ya mali, fedha na rasilimali za chama hadi watakapotekeleza matakwa ya sheria;
-
Iamuru wadaiwa walipe gharama za kesi hiyo;
-
Itoe nafuu nyingine yoyote ambayo Mahakama itaona kuwa inafaa.
Awali, Mahakama ilikubaliana na maombi ya walalamikaji kwa kutoa amri ya muda mnamo Juni 10, 2025, ya kuzuia CHADEMA kuendesha shughuli zake za kichama, matumizi ya mali za chama na ushiriki wa viongozi wake katika shughuli za kisiasa, hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Shauri la maombi ya kumkataa Jaji Mwanga pamoja na ombi la kuondoa amri za Mahakama, linatarajiwa kusikilizwa Julai 14, 2025, ambapo pande zote zitawasilisha hoja zao mbele ya Mahakama.

0 Comments:
Post a Comment