Serikali Yatangaza Mafunzo kwa Mabloga kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025: Wadau Wataka Weledi na Uwajibikaji Katika Uandishi wa Kidijitali


Katika hatua muhimu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, Serikali imetangaza kutoa mafunzo maalum kwa mabloga kote nchini, ikiwa ni juhudi za kuimarisha weledi na uwajibikaji wa watoa maudhui ya kidijitali katika usambazaji wa habari sahihi.



Tangazo hilo limetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, wakati wa Mkutano wa Wadau wa Habari uliofanyika Julai 9, 2025 katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

Katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Chama cha Mabloga Tanzania (TBN), Beda Msimbe, alisisitiza umuhimu wa kuwajengea uwezo mabloga kuelekea uchaguzi kwa kusema:

“Wao wanabeba dhamana kubwa kutokana na wingi wao na wanatengeneza maudhui, na wengine si waandishi wa habari.”

Msimbe alieleza kuwa blogu na tovuti ndizo zimekuwa chanzo kikuu cha habari kwa wananchi wengi katika zama hizi za teknolojia, akisisitiza kwamba mafunzo hayo yatasaidia kudhibiti upotoshaji na kuchochea uwajibikaji wa mabloga:

“Katika dunia ya sasa ya teknolojia na akili bandia (AI), habari zinazotegemewa zaidi si mitandao ya kijamii, bali maandishi yanayopatikana kwenye blogu na tovuti.”

Kwa mujibu wa Msigwa, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeelekezwa kuandaa mafunzo hayo mapema iwezekanavyo, ili kuhakikisha kuwa mabloga wanapata maarifa sahihi kuhusu uandishi wa habari, sheria za uchaguzi, na maadili ya taaluma hiyo.

“Mabloga wamekuwa sehemu kubwa ya mfumo wa habari. Tunapaswa kuwajengea uwezo kwa sababu nafasi yao katika uchaguzi huu ni muhimu kama ilivyo kwa waandishi wa habari wa kawaida,” alisema Msigwa.

Mkutano huo ulifunguliwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, ambaye alihimiza vyombo vya habari, mabloga, na taasisi za usalama kushirikiana kulinda amani, uvumilivu na mshikamano wa kitaifa kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Nafasi ya AI: Faida na Tahadhari

 Akili bandia (AI) ina nafsi p⁰katika kusaidia kazi za habari na utengenezaji wa maudhui. AI inaweza kusaidia mabloga kwa:

Kuchambua habari haraka na kutoa mifumo ya muhtasari yenye ubora
Kusaidia kutafsiri lugha na kuongeza upatikanaji wa habari kwa jamii pana
Kugundua taarifa potofu na kuzipatia marekebisho kabla ya kuchapishwa

Hata hivyo, wadau walionya kuwa matumizi mabaya ya AI yanaweza kuathiri uhuru na usahihi wa habari, hasa pale inapotumika:

Kusambaza habari za kughushi (deepfakes)
Kutengeneza propaganda au uchochezi kwa kutumia “bots”
Kuharibu uhalisia wa taarifa kwa kuchanganya ukweli na uongo kwa ustadi mkubwa

“AI ni silaha ya pande mbili. Inaweza kusaidia kuboresha kazi ya habari, lakini pia inaweza kutumika vibaya kuvuruga uchaguzi na kueneza taharuki,” alionya mmoja wa wachangiaji wa mkutano huo.


Hatua ya Serikali kutambua mchango wa mabloga ni ya kihistoria, na inaonesha mwelekeo mpya wa kuthamini uandishi wa kidijitali kama nguzo muhimu ya demokrasia. Mafunzo yatakayotelewa yataimarisha uwezo wa mabloga zaidi ya 200 walio ndani na nje ya Tanzania wanaowakilishwa na TBN, na kusaidia kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani, ukweli na haki ya taarifa.


0 Comments:

Post a Comment