MACHINGA WAMEPEWA WIKI MBILI KUONDOKA KARIAKOO KUPISHA UZINDUZI WA SOKO JIPYA

 

Wafanyabiashara wadogo maarufu kama machinga waliopo pembezoni mwa barabara eneo la Kariakoo, jijini Dar es Salaam, wamepewa muda wa wiki mbili kuondoka katika maeneo hayo na kurejea kwenye maeneo rasmi waliopangiwa ili kupisha maandalizi ya uzinduzi wa soko jipya la Kariakoo.



Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Mei 28, 2025, kuhusu maendeleo ya ujenzi wa soko jipya, ambalo limekamilika kwa zaidi ya asilimia 98.

“Soko limeshakamilika kwa asilimia 98, hivyo natoa muda wa wiki mbili kuanzia leo, Mei 28, 2025, kwa machinga waliopo barabarani Kariakoo kuondoka na kwenda maeneo waliyopangiwa,” alisisitiza RC Chalamila.

Alieleza kuwa lengo la hatua hiyo ni kufungua njia za kuingilia bidhaa kuelekea kwenye soko jipya ili shughuli za kibiashara zifanyike kwa ufanisi zaidi pindi litakapozinduliwa.

Chalamila pia alitoa hakikisho kwa wafanyabiashara waliokuwepo katika soko la awali kabla halijaungua, kwamba wote wamehakikiwa na watarejeshwa sokoni kama alivyoagiza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan


Aliongeza kuwa wafanyabiashara hao watalazimika kujaza mikataba na kulipa kodi ili kupata nafasi zao kihalali kupitia mfumo wa kisasa.

“Wote waliokuwepo wamehakikiwa, watarudishwa sokoni, na sasa hakuna tena udalali wa upangishaji maeneo. Tumefanikisha hilo kwa kutumia mfumo wa kidijitali wa TAUSI,” alibainisha Chalamila.


 

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko Kariakoo, Ashraph Abdulkarim, alisema kuwa shirika linaendelea kuratibu urejeo wa wafanyabiashara waliokuwepo awali kwa kuzingatia mpangilio wa biashara.

“Mpaka sasa, wafanyabiashara 1,150 kati ya 1,520 waliohakikiwa tayari wamesajiliwa kupitia mfumo wa TAUSI ili kuanza kurejea sokoni,” alisema Abdulkarim.

Aliongeza kuwa maeneo mengine ya wazi yaliyosalia yatatangazwa kupitia mfumo huo ili kutoa fursa kwa wapangaji wapya kwa uwazi na usawa.

Hatua hii ya serikali inalenga kuboresha mazingira ya biashara, kurasimisha shughuli za kiuchumi na kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wote wanapata huduma bora katika soko la kisasa la Kariakoo, ambalo lina matarajio ya kuwa kitovu kikuu cha biashara jijini Dar es Salaam.

0 Comments:

Post a Comment