Bilionea maarufu wa teknolojia, Elon Musk, ametangaza rasmi kujiuzulu kutoka nafasi yake ya Mfanyakazi Maalum wa Serikali ya Marekani alikokuwa akiiongoza Idara ya Ufanisi wa Serikali (DOGE), akilalamikia mswada mpya wa matumizi uliopitishwa na Rais Donald Trump.
Musk, ambaye aliteuliwa kuongoza juhudi za kupunguza matumizi ya serikali kwa kutumia mbinu za kiteknolojia na kufuta nafasi zisizo na tija, amesema kuwa mswada huo mpya unavuruga juhudi zote za mageuzi serikalini.
“Nilivunjika moyo kuona mswada mkubwa wa matumizi, ambao kimsingi unaongeza nakisi ya bajeti na kuharibu kazi ambayo timu ya DOGE ilikuwa inafanya,” alisema Musk katika mahojiano na CBS News.
Kupitia mtandao wake wa kijamii, X (zamani Twitter), Musk alieleza kuwa muda wake serikalini umetimia, lakini akaongeza kuwa sababu kubwa ya kujiuzulu ni kuvunjwa kwa dira ya kimfumo ya DOGE.
“Ninamshukuru Rais Trump kwa fursa ya kihistoria ya kujaribu kupunguza matumizi yasiyo ya lazima serikalini, lakini juhudi zetu zimevurugwa na mswada huu,” aliandika Musk.
Mswada wa matumizi uliopitishwa na Bunge la Wawakilishi wiki iliyopita umeelezwa kuongeza nakisi ya bajeti kwa kiasi kikubwa. Ingawa serikali ya Trump imejaribu kupunguza athari za kisiasa za hatua hiyo, migawanyiko ndani ya utawala huo imeanza kujitokeza wazi.
Naibu Mkuu wa Utumishi wa Umma, Stephen Miller, alisema kuwa:
“Mswada huo mkubwa hauhusiani moja kwa moja na bajeti ya kila mwaka, na mageuzi ya DOGE yatatekelezwa kupitia mswada tofauti.”
Musk aliteuliwa na Trump mwaka 2024 baada ya kushinda uchaguzi, na alipewa jukumu la kusimamia mageuzi ya kiutendaji ndani ya taasisi za serikali kupitia DOGE – idara maalum iliyoundwa kwa lengo la kupunguza urasimu, kuongeza tija, na kurahisisha huduma kwa raia.
Hata hivyo, ndani ya kipindi kifupi, DOGE ilijikuta katika moto wa kisiasa. Maelfu ya wafanyakazi wa umma walifutwa kazi, idara nyingi kufungwa, huku maandamano yakiibuka katika miji mikuu ikipinga kile kilichoelezwa kuwa "sera za kiimla dhidi ya tabaka la kati na chini."
Katika moja ya maandamano makubwa yaliyofanyika Washington Machi 4, 2025, wananchi walipaza sauti dhidi ya DOGE na hatua za kiutendaji zilizoongozwa na Musk, ambapo baadhi ya waandamanaji walichoma magari ya Tesla kama ishara ya upinzani.
“Watu walikuwa wanachoma magari ya Tesla – hilo halikuwa jambo la kiungwana kabisa,” alisema Musk katika mahojiano na The Washington Post.
Katika hotuba yake ya kuaga, Musk alisema:
“Mpango wa DOGE utaendelea kuimarika kwa muda kama sehemu ya maisha ya kila siku ya serikali, lakini pia ni wazi kuwa imekuwa dampo la lawama kwa matatizo yasiyohusiana nayo moja kwa moja.”
Musk pia alifichua kuwa biashara zake ziliathirika kutokana na jukumu lake la serikali:
“Ukweli ni kwamba, urasimu wa serikali ya Marekani ni mbaya zaidi kuliko nilivyodhani. Nilijua kuna matatizo, lakini kupambana kuboresha mambo DC ni kama kupanda mlima wa barafu.”
Kwa sasa, Musk amesema atarudi kujikita zaidi katika shughuli zake binafsi hasa kwenye makampuni ya Tesla, SpaceX, na Neuralink, kufuatia mlipuko wa roketi ya Starship wiki hii juu ya Bahari ya Hindi.
Aidha, bilionea huyo amedokeza kupunguza matumizi yake ya kifedha katika siasa, licha ya kuwa mmoja wa wafadhili wakubwa wa kampeni ya chama cha Republican mwaka 2024 ambapo inakadiriwa alitumia zaidi ya dola milioni 250 kumsaidia Trump kurejea madarakani.
Kujiuzulu kwake kunachukuliwa na wachambuzi kama ishara ya mgawanyiko mkubwa kati ya Musk na Trump, licha ya ushirikiano wao wa awali uliokuwa wa karibu.
Vyanzo: DW, AFP, DPA, CBS News, Washington Post, X (Elon Musk)

0 Comments:
Post a Comment