Shirika la Masoko ya Kariakoo limetangaza kuwa mnada wa wazi wa nafasi za biashara katika soko jipya la Kariakoo utafanyika kuanzia Juni 2, kupitia mfumo wa TEHAMA uitwao TAUSI, baada ya ukarabati wa soko hilo kufikia asilimia 98 ya kukamilika.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Meneja Mkuu wa Shirika hilo, CPA Ashiraph Yusuph Abdulkarim, amesema kuwa hatua hii inalenga kutoa fursa kwa wafanyabiashara wapya kuingia sokoni huku waliokuwepo awali wakiendelea kurejeshwa.
“Natoa wito kwa wananchi wote, taasisi za umma na binafsi kuchangamkia fursa ya kupata maeneo ya kufanya biashara katika soko jipya la Kariakoo kwani bado kuna maeneo ya wazi yanahitaji kujazwa baada ya kuwa tumewarejesha wale wa awali waliokuwepo,” amesema CPA Abdulkarim.
Kwa mujibu wa CPA Abdulkarim, kati ya wafanyabiashara 1,520 waliokuwa sokoni kabla ya ukarabati, hadi sasa ni wafanyabiashara 1,159 waliokamilisha usajili kupitia mfumo wa TAUSI. Wafanyabiashara wengine 361 bado hawajapangiwa kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo:
-
134 ambao taarifa zao za urithi na tofauti ya majina na namba za NIDA/TIN hazijakamilika,
-
8 ambao hawajasajili kabisa kwenye mfumo wa TAUSI,
-
19 wenye makampuni au vikundi ambavyo havijakamilisha taarifa,
-
102 ambao hawajajitokeza kujaza fomu,
-
98 ambao bado wanadaiwa madeni na Shirika.
CPA Abdulkarim pia alieleza kuwa mradi huo umetekelezwa kwa ufanisi mkubwa kwa ufadhili wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania:
“Tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia zaidi ya shilingi bilioni 28 zilizofanikisha mradi huu wa kimkakati,” alisema.
Soko jipya la Kariakoo lina jumla ya sakafu 8 zenye maeneo 1,357, yakiwemo vizimba 764, maeneo 441, na ramps 152.
CPA Abdulkarim alifafanua kuwa upangaji wa maeneo umegawanywa kulingana na aina ya biashara na sakafu, ambapo kila sakafu imepangiwa biashara maalum kwa lengo la kuongeza ufanisi na utaratibu katika shughuli za kibiashara.
Mpangilio wa Sakafu:
-
Sakafu ya chini ya ardhi: Maegesho ya magari, maghala na ‘cold rooms’.
-
Sakafu ya ardhi hadi ya pili: Biashara ya mazao mabichi.
-
Sakafu ya tatu hadi ya tano: Vifungashio, nafaka, viungo vikavu, viuatilifu, pembejeo za kilimo, mizani, cherehani, huduma za afya na tiba mbadala.
-
Sakafu ya sita: Migahawa ya chakula na vinywaji.
-
Ramps: Kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo (machinga).
Aidha, soko pia lina maeneo mengine 550 yenye biashara kama ‘Shimoni Cold Rooms’, stoo, na eneo la wafanyabiashara wa jumla wa matunda.
Katika sakafu ya chini na ya kwanza, kutakuwa na huduma kama:
-
ATM na benki,
-
Bucha za nyama na samaki,
-
Fremu za mawakala,
-
Biashara za nguo, viatu, vitenge na mashuka,
-
Huduma za vifaa vya simu, stationery, bidhaa asilia, na ofisi za kukodi.
CPA Abdulkarim alisema kuwa mpango wa kuwarejesha wafanyabiashara utafanyika kwa awamu, kulingana na ukamilifu wa maeneo na aina ya biashara zinazotarajiwa kufanyika.
Kwa ujumla, alisema:
“Mradi huu unatarajiwa kuleta fursa zaidi ya ajira 4,000 kwa Watanzania, kuongeza mapato ya Serikali na kuboresha mazingira ya kufanyia biashara jijini Dar es Salaam.”
Kwa wafanyabiashara na wawekezaji, huu ni mwito wa kipekee kuchangamkia nafasi katika soko la kisasa, lenye miundombinu ya hali ya juu na mpangilio uliolenga ustawi wa biashara na uchumi wa Taifa.

0 Comments:
Post a Comment