Baada ya Ubalozi wa Marekani Kutoa Angalizo kwa Raia Wake
Jeshi la Polisi Tanzania limetolea ufafanuzi taarifa kuhusu tahadhari ya usalama iliyotolewa na Ubalozi wa Marekani, ikieleza kuwa hakuna tishio kubwa la usalama katika maeneo ya visiwani na pwani kusini mwa Kisiju.
Taarifa hiyo imekuja muda mfupi baada ya Ubalozi wa Marekani kutoa angalizo kwa raia wake kuepuka kutembelea maeneo hayo bila idhini maalum.
Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, David Misime alizungumza na vyombo vya habari, akisema, "Tunawataka wananchi kuendelea kufanya shughuli zao kwa amani na utulivu. Nchi yetu iko salama na tunahakikisha usalama wa wananchi na wageni. Hata hivyo, tunafuatilia kwa karibu taarifa zinazoenea kuhusu uwepo wa tishio la kiusalama katika maeneo ya ukanda wa Pwani, hususan maeneo ya Kusini mwa Kisiju."
Awali, tarehe 21 Machi 2025, Ubalozi wa Marekani ulitoa tahadhari kwa raia wake kuhusu hatari inayoweza kutokea katika maeneo ya visiwani na pwani ya Kusini mwa Kisiju, Tanzania.
Taarifa ya ubalozi ilisema, "Raia wa Marekani wanapaswa kuepuka kutembelea maeneo ya visiwa na pwani, hususan kusini mwa Kisiju, bila idhini maalum."
Kwa sasa, Jeshi la Polisi limesisitiza kuwa hali ya usalama inafuatiliwa kwa karibu, na hakuna tishio kubwa linaloashiria hatari kwa raia.
Taarifa ya Marekani iliwataka raia wake kuwa waangalifu, kuendelea kufuatilia vyombo vya habari vya ndani kwa taarifa zaidi, na kuwa na tahadhari katika maeneo yanayohusisha utalii.
Hatua za Kuchukua:
- Epuka eneo hilo.
- Fuata vyombo vya habari kwa taarifa zaidi.
- Wasiliana na familia na marafiki kuhusu usalama wako.
- Kuwa makini na mazingira yako.
- Rejea mipango yako ya usalama wa kibinafsi.
- Kuwa macho katika maeneo yanayotembelewa na watalii.

0 Comments:
Post a Comment