Balozi Daniel Ole Njoolay: “Safari Yangu ni Muujiza wa Elimu, Uongozi na Utumishi kwa Taifa”

 



Katika hafla ya uzinduzi wa kitabu chake Tawasifu ya Balozi Daniel Ole Njoolay, iliyohudhuria na viongozi mbalimbali wakiwemo Mgeni Rasmi, Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Habari; pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, James Millya, Balozi Daniel Ole Njoolay alitoa risala yenye kugusa hisia kuhusu maisha yake, safari ya elimu na utumishi wake kwa umma.



Balozi Ole Njoolay alieleza kuwa chanzo cha kitabu hicho:
“Uamuzi wa kuandika kitabu hiki nilichukua miaka mitatu iliyopita, baada ya msukumo wa marafiki wengi ambao kwa muda mrefu walinishauri kufanya hivyo. Baadhi yao wapo hapa leo. Kitabu hiki kinaeleza maisha yangu na utumishi wangu kwa umma, safari ambayo kwa sehemu kubwa imejaa miujiza.”

Safari ya Elimu Katika Mazingira Magumu



Balozi Njoolay alisimulia changamoto za kupata elimu katika jamii ya Kimasai kipindi hicho, ambako wazazi walikataa watoto kwenda shule wakiamini ni sawa na ‘kuwapoteza’.

“Wazee walipokubaliana angalau kila boma litoe mtoto mmoja, mzazi alichagua mtoto ambaye si ‘rasilimali kubwa sana’. Mimi nilichaguliwa kwa sababu nilikuwa sichungi mbuzi vizuri,” alisema kwa utani uliochekesha ukumbi.


Alieleza kuwa alipoanza shule, mzazi alilazimika kulipa ada mwaka mmoja baada ya kuanza masomo. Baada ya baba yake kufariki dunia, watu walimwambia mama yake aache kumsomesha kwa kuwa alikuwa mjane.
“Hata hivyo, mama yangu hakukata tamaa. Nilipofaulu kwenda sekondari, aliniuliza kama nataka kuendelea. Nilimwambia ndiyo, akaniambia basi tuuze ng’ombe iliyobaki. Huo ndio ulikuwa msingi wa safari yangu.”

Uongozi Bila “Godfather”



Akimweleza hadhira jinsi alivyoingia kwenye uongozi, Balozi Njoolay alisema matukio mengi katika maisha yake yalikuwa ya kipekee.
“Nilishinda ujumbe wa NEC (Vijana) nikiwa na miaka 29. Nilikuwa mgeni kabisa ndani ya chama, lakini nikaomba kura kwa mara ya kwanza na nikachaguliwa,” alisema.

Aliendelea kueleza kuwa uteuzi wake kuwa Mkuu wa Mkoa kwa miaka 16 ulikuwa “maajabu mengine”, na zaidi ni uteuzi wake kuwa Balozi licha ya kutokuwa mwanadiplomasia kwa taaluma.
“Walioniteua waliridhika na utendaji wangu, na wananchi waliridhika na utendaji wangu. Huo ndio ulikuwa msingi wa safari yangu ya uongozi.”

Shukrani kwa Mwandishi

Katika risala hiyo, Balozi Njoolay alimpongeza na kumshukuru mwandishi mkongwe wa habari, Bw. Hassan Hassan.
“Amebeba jukumu kubwa katika uandishi wa kitabu hiki. Amefanya kazi kwa uadilifu na umakini mkubwa,” alisema.

Wito kwa Vijana na Wasomaji

Balozi Njoolay alisema lengo lake kuu ni kuwainua na kuwapa dira vijana wa sasa, hasa wale wanaotamani kutumikia taifa.
“Baadhi ya watu walinisukuma kuyaandika haya ili viongozi vijana wapate kujifunza. Ni imani yangu kwamba mtafurahia kukisoma na huenda mkafaidika nacho. Mungu awabariki sana,” alihitimisha.

Uzinduzi huo uliendelea kwa furaha na tafakuri, huku hadhira ikionyesha kuthamini mchango wa Balozi Ole Njoolay—kiongozi ambaye safari yake ni somo la ujasiri, kujituma na uaminifu katika utumishi wa umma.


0 Comments:

Post a Comment