Happy Lazaro,Arusha .
SHULE ya mchepuo wa kiingireza ya Dominion Pre &Primary kwa kushirikiana na Ecobank pamoja na shirika la Enkitoria Foundation kwa pamoja wameungana na kutoa msaada wa vitu mbalimbali katika kituo cha kulelea watoto waishio mazingira magumu cha Rescue Children Charity Organization kilichopo jijini Arusha .
Akizungumza wakati wa kukabithi misaada hiyo Mkurugenzi wa shule hiyo ,Florentina Kazawadi amesema kuwa,wamefikia hatua ya kusaidia kituo hicho baada ya kuona uhitaji walio nao ili na wenzao waweze kuona wana watu wa kuwasaidia ambapo wamekabithi mafuta ya kupikia, sabuni, Michele, unga, nguo, maharage, sukari pamoja na tambi.
Florentina amesema lengo la shule hiyo kutoa misaada hiyo kwenye kituo hicho ni ili kuwasaidia watoto hao kuondokana na changamoto mbalimbali huku akiitaka jamii ijikite kusaidia na kuhurumiana badala ya kutegemea msaada kutoka nje kwani ni jambo zuri endapo watasaidiana wenyewe kwa wenyewe .
Amefafanua kuwa ,walianza kuchukua watoto wanaotoka kwenye mazingira magumu ambapo walichukua watoto watatu kwa kila darasa na kuwasomesha shuleni hapo ambapo hadi sasa hivi wamesomesha watoto 51 ambapo wengine wapo vyuoni na wengine wanaendelea hapo shuleni.
Amesema kuwa,baada ya kuona changamoto nyingi zinazowakabili watoto wanaotoka kwenye mazingira magumu mwaka 2023 walianzisha shirika lisilo la kiserikali la Enkitoria Foundation kwa lengo la kusaidia watoto hao kwa karibu na kuweza kuwafuatilia na kuwasaidia mahitaji mbalimbali .
"Tulianza kufanya ziara vijijini kwa watoto wanaotoka katika jamii ya kifugaji wilayani Simanjiro na kuweza kuwapa mahitaji mbalimbali ikiwemo vifaa vya shule, chakula pamoja na taulo za kike na vifaa vya usafi kama sabuni kwa wanafunzi wa jamii ya kifugaji wapatao 97 ."amesema .
Ameongeza kuwa, shirika hilo limeweza kufika pia wilayani Loliondo kwa shule ya serikali na kutembelea watoto mpaka waliopo majumbani na kuwapatia mahitaji mbalimbali .
Aidha ametoa wito kwa wadau mbalimbali kujenge utamaduni wa kusaidiana na kuhurumiana wenyewe kwa wenyewe kwa kile kidogo walichonacho kwani watoto hao wana mahitaji mengi sana hivyo ni wajibu wetu kushikana mkono na kuwasaidia .
Kwa upande wake Mwanzilishi msaidizi wa shirika la Enkitoria Foundation, Abiud Wanakai lengo la shirika hilo ni kusaidia watoto wanaotoka kwenye mazingira magumu ambapo amesema ndoto yao wataendelea kusaidia kituo hicho katika kuondokana na changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Aidha amewataka wadau mashirika na watu binafasi wawe na ndoto ya kufanya matendo ya huruma mara kwa mara kwani ukifanya jambo Mungu naye anakukumbuka pia,huku akiwataka kuwa na moyo wa utu na kuinuana ili kusiwepo na utofauti kwenye maisha .
Mwanzilishi wa kituo hicho ,Tumaini Erasto amesema kuwa kituo hicho kilianza rasmi mwaka 2021 kikiwa na watoto 3 ambapo hadi sasa hivi wana jumla ya watoto 19 ambapo wasichana ni 12 na wavulana 6 ambapo amesema wamekuwa wakipambana wenyewe kuwapatia mahitaji mbalimbali huku wakiomba wadau mbalimbali kujitokeza kuwasaidia kwani mahitaji ni mengi .
Aidha Tumaini amewashukuru sana kwa misaada hiyo huku akiwaomba jamii kujitokeza kuwasaidia ujenzi wa madarasa kwani darasa lililopo limechakaa pamoja na ukosefu wa kiwanja kwa ajili ya kujenga mabweni huki wakiomba kujengewa uzio kwa ajili ya ulinzi wa watoto kwani uliopo ni wa mabati na ni hatari kwa watoto hao sambamba na kuomba wadau wajitokeze kwa ajili ya kupata chakula cha watoto hao .
Naye Mmoja wa wazazi mwakilishi wa watoto wa shule ya Dominion Anna Kinunda amesema kuwa, anashukuru uongozi wa shule hiyo kwa wazo hilo huku akiomba iwe mfano kwa shule nyingine kwani matendo ya huruma yanatakiwa yafanyike kila siku hivyo ni vizuri wakaiga mfano wa shule hiyo katika kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalumu.
Mmoja wa watoto hao wanaolelewa kwenye kituo hicho ,ameshukuru shule hiyo kwa msaada huo waliopatiwa kwani wengi wa watoto hawana wazazi wanategemea misaada kutoka kwetu.
0 Comments:
Post a Comment