Mashirika ya Haki za Binadamu Yapinga Kanuni za Maudhui Mtandaoni Mahakamani: Yadai Zinakiuka Haki za Binadamu



Arusha, Tanzania – Baadhi ya vifungu vya Kanuni za Maudhui Mtandaoni chini ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) vimepingwa katika Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) vikidaiwa  kukiuka misingi ya haki za binadamu na masharti ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.



Kesi hiyo, namba 30/2020, ilisikilizwa leo Novemba 13, 2025 mbele ya jopo la majaji watano wa Mahakama ya EACJ , wakiongozwa na Jaji Johanes Masara, akisaidiwa na Majaji Richard Wejuri, Richard Muhumuza, Dkt. Gacuko Leonard, na Kayembe Kasanda.



Shauri hilo dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali linalofuatiliwa kwa karibu na wadau wengi wa haki limefunguliwa na Mashirika manne ya haki za binadamu likiwemo Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Baraza la Habari Tanzania (MCT), Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), na taasisi ya Center for Strategic Litigation.


Akiwasilisha hoja za waleta maombi, Wakili Jeremiah Mtobesya, alisisitiza kuwa Sheria yoyote inayotungwa inapaswa kuzingatia misingi ya haki za binadamu, ikiwemo uhuru wa kutoa na kupokea taarifa. Alihoji kuwa, licha ya marekebisho yaliyofanywa kwa baadhi ya vifungu vya sheria hiyo mwaka 2022 na 2025, bado vifungu namba 3, 4, 5, na 6 vina mapungufu makubwa yanayoweza kuathiri uhuru wa watu kutoa maoni yao kwenye mitandao ya kijamii.

“Vifungu hivi vinatoa nafasi ya matumizi mabaya, kwa sababu havibainishi wazi makosa yanayohusu usambazaji wa maudhui. Hii inatoa nafasi kwa mamlaka kutumia sheria hii kudhibiti uhuru wa kujieleza,” ameeleza Mtobesya.

Pia, Wakili Mtobesya alieleza kuwa adhabu ya faini ya shilingi milioni tano au kifungo cha miezi 12 kwa makosa ya kimaudhui ni kubwa na inatishia uhuru wa kujieleza, hasa kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii.



Naye , Wakili Peter Majanjala aliongeza kuwa mfumo wa utoaji wa leseni za maudhui mtandaoni unahitaji marekebisho, kwani hauzingatii tofauti kati ya watoa maudhui wa kibiashara na wale wa kijamii au binafsi. Alisema kuwa kanuni hizi pia zinakiuka masharti ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, hasa vifungu 6(d), 7, na 8(c) vinavyohusiana na demokrasia, uongozi bora, na kulinda haki za binadamu.

“Kanuni hizi zinakiuka haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na uhuru wa kujieleza, kupokea taarifa, na kutoa taarifa. Hii ni kinyume na misingi ya mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisisitiza Majanjala.

Kwa upande wa Serikali, mawakili waandamizi Stanley Kalokola na Daniel Nyakiha walijibu kuwa vifungu vya sheria vilivyolalamikiwa tayari vimefanyiwa marekebisho, na kwamba kanuni hizo hazikiuki haki za binadamu. Wakili Kalokola alisema kuwa kanuni za Maudhui Mtandaoni zinalenga kulinda maadili ya kijamii na usalama wa taifa, na si kuingilia uhuru wa watu kutoa na kupokea taarifa.

“Kanuni hizi zinawalinda raia dhidi ya usambazaji wa maudhui hatarishi. Haziingilii haki za kutoa na kupokea taarifa,” alisema Wakili Kalokola.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Jaji Johanes Masara aliahirisha shauri hilo na kusema kuwa tarehe ya kutoa hukumu itatangazwa baadaye.

Shauri hili ni mojawapo ya mashauri manne yaliyosikilizwa wiki hii katika Mahakama ya Afrika Mashariki kuhusu masuala ya haki za binadamu. Mashauri mengine ni yale yaliyofunguliwa na Chama cha Mawakili wa Afrika (PALU), THRDC, na LHRC, na shauri la Abdul Omar Nondo dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Mahakama imesema itapanga tarehe ya kutoa hukumu baada ya kuwajulisha wahusika wote.


0 Comments:

Post a Comment