Dkt. Slaa Aarejea Chadema, Aomba Msamaha Hadharani, Makamanda Wataka Kina Mdee Nao Wasamehewe



Mwanasiasa mkongwe na aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Wilbroad Slaa, amerejea tena kwenye chama hicho baada ya kuwa nje kwa takribani miaka 10. 



Dkt. Slaa amerejea ndani ya CHADEMA na kupokelewa kwa shangwe katika mkutano wa hadhara uliofanyika leo Machi 23, 2025, jijini Mbeya.


Mkutano huo ulifanyika ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa kampeni ya ‘No reform, no election’ kwa mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini. Mkutano huu ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama hicho kutoka mikoa ya taifa, wakiwemo Mwenyekiti wa Taifa, Tundu Lisu, na viongozi wa kanda mbalimbali.



Katika hotuba yake, Dkt. Slaa alielezea uamuzi wake wa kuomba radhi kwa wanachama na viongozi wa chama hicho kwa makosa aliyoyafanya alipokuwa akitangaza kuachana na siasa za Tanzania mwaka 2015. 



Alisema, "Nimeamua kuja kuwaomba radhi hadharani wanachama wa Chadema, naombeni mnisamehe kwa lolote ambalo niliwakosea na naomba mnipokee, nataka nishirikiane na nyie kwenye harakati za kulikomboa taifa letu."



Amesema moja ya mambo yaliyomvutia kurejea kwenye chama hicho ni kampeni ya ‘No reform, no election’, akidai kuwa kampeni hiyo ina lengo la kubadili mfumo wa uchaguzi kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu. 


“Chama hiki ndicho chama ambacho kimeonyesha kuwa na sera ambazo zina uwezo wa kubadili maisha ya Watanzania,” alisema Dkt. Slaa, na kuwataka Watanzania kukiunga mkono chama hicho.

Ujio wa Dkt. Slaa ulijulikana mapema wakati wa kampeni za Uchaguzi wa ndani wa chama hicho mwezi Januari mwaka huu. Hata hivyo, baadhi ya makamanda walionekana kupinga uamuzi huu, wakiwemo Mwenyekiti wa Chadema Kanda Victoria, Ezekia Wenje, ambaye alizungumzia kitabu cha Dkt. Slaa kilichosema kumhusu Tundu Lisu. 


"Mtu (Dkt. Slaa) ameandika kitabu on record ya kuchafua chama chetu kila kona," alisema Wenje, akihoji uaminifu wa Dkt. Slaa.

Pamoja na upinzani huu, mara baada ya Dkt. Slaa kuomba radhi na kupokelewa na Lisu, baadhi ya viongozi na wanachama walimwunga mkono, huku wengine wakikosoa uamuzi huo. Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa Chadema, Yericko Nyerere, aliibua hoja akitaka msamaha wa Dkt. Slaa uende kwa wote walioonekana kukiasi chama hicho, wakiwemo wabunge 19 na aliyekuwa Mwenyekiti wa BAWACHA, Halima Mdee, ambao walikosa uungaji mkono kwa kuandika katika mitandao ya kijamii wakisema, “Ninapongeza uamuzi wa kumrejesha ndani ya @ChademaTz Dr Slaa, ni uamuzi wa busara pamoja na udharimu wote aliokifanyia chama chetu. Ninashauri wote waliohama/kufukuzwa hasa @halimamdee na wenzake (COVID 19) warejeshwe bila masharti yoyote kama Slaa. Tumeamua kujenga chama upya!”

Dkt. Slaa, ambaye alisoma seminary kuu na kuwa padri wa Kanisa Katoliki, alikamilisha PhD ya Sheria huko Italia kabla ya kuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC). Alijitosa katika siasa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambapo mwaka 1995 alikatwa jina kwenye mchakato wa kugombea ubunge jimbo la Karatu hivyo akajiunga na Chadema na alikuja kuwa Mbunge. 

Hata hivyo, aliungana na juhudi za Rais John Pombe Magufuli, jambo lililosababisha baadhi ya watu kumuita msaliti. Leo, Dkt. Slaa amepokelewa tena na chama chake cha zamani na kupigiwa upatu na viongozi na wanachama wa CHADEMA.


0 Comments:

Post a Comment