MAHAKAMA YAAMURU UPELELEZI UHARAKISHWE KESI YA MAUAJI YA POLISI LOLIONDO

 



MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Arusha imeutaka upande wa Jamhuri kuharakisha upelelezi wa kesi ya mauaji inayowakabili watu 27 wakiwemo  madiwani 10, mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, (CCM), wilayani Ngorongoro ili kuwezesha wanafunzi wawili kupata haki yao ya kuendelea na masomo

 

Aidha, imetaka upelelezi huo ukamilike ili washitakiwa wengine wawili ambao ni wagonjwa mmoja anaugua kisukari na mwingine figo waweze kupatiwa haki ya matibabu huku ikionya haitakuwa jambo zuri watu hao wakifa kwani mahakama  na upande wa jamhuri kuwa sehemu ya waliosababisha kifo hicho na kuwakosesha haki ya kuishi.

 

Pia, yaliibuka mabishano makali ya kisheria mahakamani hapo baada ya mahakama kukiri kuwa Julai 5, mwaka huu ilipokea na kusikiliza maombi ya upande wa Jamhuri ya kufanyia mabadiliko hati ya mashitaka kwa kuongeza washitakiwa wawili bila kuwashirikisha washitakiwa 25 wa awali wala mawakili wao.

 

Hayo yamesemwa Leo Julai 14,2022  na Hakimu Mkazi, Herieth Mhenga ambaye shauri hilo la mauaji namba 11/2022 linatajwa mbele yake kwani mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.

 

 

Amesema kuwa ni vema upelelezi huo ukakamilika mapema ili shauri hilo likasikilizwe kwenye mahakama yenye mamlaka ili kuwezesha wanafunzi hao ambao mmoja anaingia kidato cha tano na mwingine anaendelea na mafunzo ya shahada ya uzamivu, (PHD) nchini Marekani.


Wakili wa utetezi, Jeremiah Mtobesya, ameeleza mahakama kuwa mshitakiwa wa tatu, Simel Parmwati ni mwanafunzi anayepaswa kujiunga na kidato cha tano mwaka huu na mshitakiwa wa 23, Fred Victor ni mwanachuo nchini Marekani anayepaswa kuwasilisha maandiko yake ya kitaaluma kwa wakati vinginevyo atafutiwa usajili hivyo itakuwa ni hasara kwa atakuwa amepoteza haki yake ya kupata elimu. 

 

Hakimu Mhenga alimuuliza afisa wa magereza aliyekuwa mahakamani hapo juu ya taratibu zinazoweza kutumika kuwasaidia wagonjwa walio mahabusu kwenye gerezani ambapo afisa huyo alisema kuwa daktari wa magereza ndiye mwenye jukumu la kushauri endapo mgonjwa anapaswa kupelekwa hospitali ya mkoa ya Mount Meru kwa matibabu zaidi nao huamua kutoa kibali cha mgonjwa kwenda kupata matibabu kwenye hospitali nyingine.

 

“Watu hawa wakifariki tutakuwa ni sehemu ya wawaliosababisha kifo hicho na hivyo jamhuri harakisheni upelelezi,” amesema Hakimu Mkazi Mhenga na kuongeza

 

 … Naomba kusema mwanafunzi anayetakiwa kuingia kidato cha tano na huyo wa PHD ambaye akiacha kuwasilisha mawasilisho yake ya kitaaluma (presentation) atafutiwa usajili hivyo tutawanyima haki yao ya kusoma,” alisema hakimu Mkazi Mhenga na kuongeza.

 

…Lakini tuangalie na hao wagonjwa hasahasa huyo anayefanyiwa ‘dialysis’ tunaomba hawa watu wapewe haki yao upelelezi ufanyike ili watu wapewe haki zao,”.

 

Hata hivyo alisema kuwa hoja nyingine zilizowasilishwa mahakamani hapo na mawakili wa pande zote mbili atazitolea uamuzi mdogo Julai 28, 2022 siku ambayo shauri hilo litarudi mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa.

 

 

Washitakiwa hao ni pamoja na Molongo Paschal, Albert Selembo,  Simeli Parmwati, (19) ambaye ni mwanafunzi Lekayoko Parmwati, (21) Sapati Parmwati, (30) Ingoi Olkedenyi Kanjwel, (20) Sangau Morongeti, (Morijoi Parmati, (20) Morongeti Meeki, (Kambatai Lulu,(40) na  Moloimet Yohana,(37)?

 

Wengine ni  Ndirango Senge Laizer, (52) Joel Clemes Lessonu, (54)  Simon Nairiam Orosikiria, (59)  Damian Rago Laiza, Mathew Eliakimu, (41) Luka Kursas, (49)  Taleng'o Twambei Leshoko, (37) Kijoolu Kakeya, (56)   Shengena Killel, (34) Kelvin Shaso Nairoti, (33)  Lekerenga Koyee, (68) Fred Victor (39) Wilsom Tiuwa Kiling, (32), James Mumes Taki (28), Simon Saitoti, (41), na Joseph Lukumay

 

Awali mawakili wa utetezi waliweka pingamizi mahakamani hapo mara baada ya wakili wa serikali, kutaka kuwasomea washitakiwa hati ya mashitaka ambayo ilifanbyiwa marekebisho julai 5, mwaka huu bila ya uwepo wa washitakiwa wala mawakili wao.

 

Wakili Mtobesya alidai kuwa hiyo ni kinyume cha sheria ya mwenendo wa uendeshaji wa mashauri  jinai kwani inataka hati hiyo inapofanyiwa marekebisho washitakiwa wawepo na wasomewe mashitaka yao hivyo wakaiomba mahakama hiyo washitakiwa hao wasisomewe mashitaka hayo.

 

“Kilichofanyika Julai 5, ubatili kwa sababu washitakiwa hawakusomewa shitaka wakubali au wakatae kwa hivyo tunarudi kwenye hoja yetu kuwa kule magereza hawako kihalali tokea tarehe 5 Julai  mpaka sasa kwa sababu hati halali inayowashitakiwa nayo iliondolewa mahakamani,” alisema Mtobesya.

 

Akitolea uamuzi hoja hizo hakimu Mhenga alisema kuwa ni kweli shauri hilo lilifika mbele yake Julai 5, 2022 bila bila uwepo wa washitakiwa 25 na  mawakili wao.

 

“ Upande wa mashitaka walileta maombi ya kufanyia mabadiliko hati ya mashitaka baada ya mahakama kukubali waliwasomea hati hiyo kwa washitakiwa wawili namba 26 na 27,” alisema hakimu Mhenga na kuongeza.

 

… Nimeandika mapingamizi ya pande zote lakini ninaamua hati hiyo isomwe kwa upya kwa washitakiwa wote. Mikono yangu imefungwa kwa sababu nilishaamua julai 5, 2022 kama kuna lolote ambalo upande wa utetezi wataona hawajaridhika wanaweza kuchukua hatua zaidi,”. 

 


0 Comments:

Post a Comment