Sakata la kubomolewa kwa kuta za uzio wa nyumba zinazomilikiwa kihalali na wananchi wa Kitongoji cha Olosiva, Kata ya Olorien, wilayaniArumeru, limechukua sura mpya baada ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kujitenga na zoezi hilo, huku viongozi wa mtaa wakijikanganya kuhusu uhalali wake.
Zoezi hilo lililofanyika Aprili 12, 2025, limesababisha uharibifu wa mali za wakazi waliokuwa na hati halali za kumiliki ardhi, huku wengi wakilalamika kutoshirikishwa ipasavyo kabla ya hatua hiyo kuchukuliwa.
Akizungumza na waandishi wa habari, Meneja wa TARURA Mkoa wa Arusha, Nicolas Francis, alieleza kuwa hawakuhusika kwa namna yoyote na ubomoaji huo, wala hawakuwa na bajeti kwa barabara husika katika mwaka wa fedha 2025/2026.
“Kilichotokea pale si maagizo ya TARURA. Sisi tunapopokea maombi kupitia vikao halali ya kwamba barabara inahitaji kuboreshwa, huwa tunaingiza katika mpango wa mwaka unaofuata au mwaka husika. Kwa barabara hiyo ya Kwa Idd hadi Kiranyi Sekondari, yenye urefu wa kilomita 0.6, hakuna bajeti mwaka huu. Kwa hiyo tusingeweza kutoa maagizo ya kuondoa vikwazo vyovyote,” alisema Francis.
Aidha, Francis alisisitiza kuwa TARURA haina mamlaka ya kuingilia maamuzi ya serikali za mitaa kama vikao vya vitongoji au mabaraza ya madiwani, lakini akaeleza kuwa maamuzi hayo yanapaswa kufanyika kwa kufuata taratibu sahihi.
“Sisi hatuingilii maamuzi ya serikali za mitaa. Kama kuna maamuzi yaliyochukuliwa bila kufuata vikao halali, basi mamlaka husika zifuatilie kwa mujibu wa sheria,” aliongeza.
Licha ya kauli hiyo ya TARURA, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Olosiva, Naishiye Kimani, alieleza kuwa wananchi walitekeleza maamuzi ya mkutano wa Kitongoji uliofanyika Machi 22, 2025.
“Waliohusika na ubomoaji ni wananchi wenyewe, wakitekeleza uamuzi wa mkutano wao. Sisi kama viongozi tulikuwapo kwa ajili ya kuhakikisha hakuna madhara yanayotokea. Nilimpigia simu askari wa kata aje kusaidia usalama lakini alisema alikuwa kwenye majukumu mengine,” alisema Kimani.
Alipobanwa kueleza kwa nini hakuchukua hatua kuzuia ubomoaji wa mali za watu walio na hati halali kwa mujibu wa sheria, Kimani alijibu:
“Ni kweli hizo zilizoharibiwa ni mali za wananchi wanamiliki kihalali, lakini unajua wananchi wakiamua jambo kwenye mkutano wao, si rahisi kuwazuia.”
Hata hivyo Kimania aliwashauri wananchi waliopo karibu na barabara kuondoka kwa hiari kupisha ujenzi wa mitaro ya maji ya mvua, huku akifichua kuwa bado kuna mpango wa kuwaondoa wengine.
Naye Maiko Mollel, Balozi wa Shina Namba 4 la CCM, alithibitisha kuwa jumla ya nyumba tano katika eneo lake zilivunjiwa kuta zao huku akidai kuwa wananchi walipewa taarifa mapema lakini baadhi yao walikaidi.
“Mimi mwenyewe nilipeleka barua zaidi ya mara tatu kwa baadhi ya wananchi warudishe nyuma kuta zao. Wapo waliotekeleza, lakini wengine walikaidi. Mwisho wa siku, wananchi waliamua kuchukua hatua,” alisema Mollel.
Alimtaja James Lukumai kama mmoja wa waliokataa kuondoa ukuta wake licha ya kushauriwa mara kadhaa na viongozi wa mtaa.
“Tulikwenda naye hadi na Mwenyekiti, tukamweleza umuhimu wa kuondoa ukuta wake, lakini hakusikia. Ilibidi wananchi wachukue hatua.
Siku hiyo tulikuwa na mabalozi 24 kwa ajili ya usalama, maana baadhi ya kuta za nyumba zilikuwa na umeme kwani wamiliki wa nyumba hizo ni wafanyabiashara,” alisema Mollel.
Soma zaidi
https://habaritanzaniagracemacha.blogspot.com/2025/04/tumeachwa-nje-kama-wakimbizi-wakazi-wa.html




0 Comments:
Post a Comment