Serikali ya Tshisekedi Yampekua Kabila, Mvutano Waongezeka

 


Maafisa wa usalama nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamevamia na kufanya upekuzi katika mali za rais wa zamani wa nchi hiyo, Joseph Kabila, ikiwa ni pamoja na shamba lake la Kingakati lililoko karibu kilomita 80 kutoka mji mkuu, Kinshasa, pamoja na nyumba yake mjini humo.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na familia ya Kabila, upekuzi huo ulifanyika jana jioni na maafisa wa usalama waliomfahamisha msimamizi wa shamba hilo kuwa ni zoezi la kawaida. Hata hivyo, familia hiyo imesema kuwa "maafisa hao walidai kuwa wanatafuta vifaa vya kijeshi vilivyoibwa au kupotea", lakini hawakufanikiwa kupata chochote.

Uvamizi huo umetokea siku chache tu baada ya Kabila kutangaza nia ya kurejea nchini kupitia upande wa mashariki wa Kongo, eneo linalokumbwa na mapigano kati ya waasi wa M23 na majeshi ya serikali. 


Hatua hiyo imezua hisia kali, huku Rais Félix Tshisekedi akimtuhumu Kabila kuwa "anapanga njama za kuiangusha serikali" na pia "kuwaunga mkono waasi wa M23 wanaopambana na vikosi vya serikali mashariki mwa Kongo".

Katika makala ya maoni iliyochapishwa kwenye gazeti la The Sunday Times la Afrika Kusini, Kabila amejibu tuhuma hizo kwa ukali, akisema kuwa hali ya machafuko mashariki mwa nchi "haiwezi kulaumiwa tu kwa waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda". 


Aliongeza kuwa "utawala mbaya wa mrithi wake, Rais Félix Tshisekedi, umechangia pakubwa katika kuzidisha mgogoro mashariki mwa nchi hiyo".

Kabila pia amekosoa vikali uchaguzi wa Disemba 2023 uliomrejesha Tshisekedi madarakani kwa muhula wa pili, akisema kuwa "uchaguzi huo ulikumbwa na udanganyifu" na kuishutumu serikali kwa "kuzima sauti za upinzani".

Aidha, alieleza kuwa tangu Tshisekedi achukue madaraka mnamo mwaka 2019, "hali nchini humo imezidi kuzorota hadi kufikia kiwango cha karibu kusambarika kabisa".

Mvutano huu wa kisiasa unaonekana kuchochea zaidi sintofahamu katika taifa hilo ambalo tayari linakabiliwa na changamoto nyingi, hasa mashariki mwa nchi ambako mapigano yanaendelea na wakazi wakiendelea kutaabika.

0 Comments:

Post a Comment