WASHITAKIWA WAOMBA KUPEWA MAKOSA YENYE DHAMANA, MMOJA ANA UGONJWA WA MOYO MWINGINE mtoto anatambaa magereza

 


MSHTAKIWA wa tatu,  John Maduhu katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili pamoja na aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Dk John Pima, ameuomba  upande wa jamhuri uwafikirie  kuwabadilishia mashitaka kwa kuwaondolea yale yasiyo na dhamana kwani anasumbuliwa na ugonjwa wa moyo.


Aidha, Mshitakiwa mwingine, Mariam Mshana ambaye alikuwa Mkuu wa Idara ya fedha katika halmashauri hiyo,  ameiomba mahakama iangalie uwezekano wa kuwapatia dhamana katika kesi nyingine mbili zinazowakabili  ili waachiwe kwa dhamana na kesi hii isiyo na dhamana waletwe mahakamani upelelezi utakapokamilika kwani ana mtoto anayetambaa kwenye mazingira ya mkusanyiko gerezani.


Mtuhumiwa huyo ambaye alikuwa  Mkuu wa Idara ya Mipango ya uchumi wa halimashauri hiyo ametoa ombi hilo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha,Fadhil Mbelwa, ambaye  shauri la uhujumu uchumi namba 5/2022 lilitajwa mbele yake.


Shauri hilo lilikuja mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa ambapo upande wa jamhuri uliwakilishwa na Wakili wa Serikali,  Charles Kagilwa, huku utetezi ukiwakilishwa na Wakili Sabato Ngogo.

 

Mara baada ya Wakili Serikali,  Kagilwa kuieleza mahakama kuwa shauri hilo lilipangwa kwa ajili ya kutajwa na kuwa upelelezi wake haujakamilika, mshitakiwa, Maduhu alisimama na kuomba upande wa mashtaka uwafikirie katika kesi hiyo ambayo haina dhamana.

 

"Nina tatizo la moyo umepanuka nahitaji mazingira yenye amani, ningeomba mwendesha mashitaka atufukirie shtaka la nne na tano ikipendeza libadilishwe tupate dhamana,"aliomba Maduhu mahakamani hapo.

 

Akijibu hoja hizo,Wakili Kagilwa,alisema kwa sasa hana la kusema ila watajitahidi kukamilisha upelelezi.

 

Kwa upande wake mshitakiwa, Mariam aliieleza mahakama hiyo kuwa wanajua kesi hiyo upelelezi haujakamilika na ndiyo inawaweka mahabusu  muda wote hivyo mahakama iangalie  utaratibu wapewe dhamana kwenye kesi nyingine mbili zinazowakabili na waletwe katika kesi hiyo wakati upelelezi wake umekamilika.

 

"Mahakama iangalie mtoto anatambaa, mkusanyiko wa magereza hivyo iangalie tupate dhamana kwa kesi zile mbili ili tuachiwe na hii moja tuletwe wakati upelelezi umekamilika kwani mazingira ya magereza mtoto anayetambaa inabidi muda wote uwe umembeba," aliomba Mariam.

 

Hakimu mkazi, Mbelwa alimweleza mtuhumiwa huyo kuwa kuna baadhi ya makosa suala la dhamana linaweza kuzungumzwa ila baadhi ya makosa dhamana yake ni changamoto.

 

"Kuna baadhi ya makosa dhamana yake ni chagamoto,ni kumuomba Mungu kesi iishe. Katika kesi hii ya tatu shitaka la tano ndilo linalofanya kesi yenu inakosa dhamana.

Kwa hiyo kwenye shtaka hilo aina cha kusema lakini tu ni rai kwa jamhuri kuharakisha upelelezi,"alisema Hakimu.

 

Washitakiwa hao watatu, wanakabiliwa na makosa sita ikiwemo kosa la utakatishaji fedha Sh103 milioni,ambapo wanadaiwa kujipatia fedha hizo huku wakijua ni zao la uhalifu la kosa la kutumia nyaraka kumdanganya mwajiri wao.

 

Awali mahakama hiyo iliahirisha kesi zingine mbili za uhujumu uchumi zinazowakabili watuhumiwa hao na wenzao wawili, kutokana na Wakili wa Serikali anayesikiliza shauri hilo kudaiwa kuwa ni mgonjwa.

 

Katika kesi ya uhujumu uchumi namba 3/2022,watuhumiwa ni Dk Pima,Mariam,Maduhu na Nuru Ginana aliyekuwa Mchumi wakitetewa na mawakili Ngogo na Joshua Minja.

 

Wakili wa serikali, Kagilwa alidai shauri lilipangwa kwa ajili ya kuwasomea hoja za awali lakini waomba tarehe nyingine kwani wakili anayewakilisha jamhuri katika kesi hiyo anaumwa.

 

Wakili Ngogo aliiomba mahakama tarehe itakayotajwa kwa washitakiwa hao waweze kusomewa maelezo hayo ya awali  kwani ni mara ya pili shauri hilo linapangwa kwa ajili ya kuwasomea maelezo hayo ya awali ila hawajaweza kusomewa.

 

Wakili Minja anayemtetea mshitakiwa wa nne(Ginana),aliieleza mahakama kuwa dhamana ya mshitakiwa huyo iko wazi na wadhamini wako mahakamani hapo ambapo upande wa jamhuri haukuwa na pingamizi baada ya kufanya uhakiki wa nyaraka husika.

 

Mshitakiwa huyo alidhaminiwa na wadhamini wawili ambapo baada ya kukidhi masharti ya dhamana Hakimu huyo alimweleza mshitakiwa huyo kuwa taratibu za dhamana zikikamilika ataachiwa kwa dhamana,ambapo wadhamini hao watapaswa kujaza fomu.

 

Katika shauri la uhujumu uchumi namba 4/20222 linalowakabili Dk Pima,Mariam,Maduhu na Alex Daniel, aliyekuwa mchumi wa jiji hilo,wakili Kagilwa aliieleza mahakama kuwa shauri hilo pia lilipangwa kwa ajili ya kuwasomea hoja za awali washitakiwa hao ila wakili anayehusika na shauri hilo ni mgonjwa.

 

 

Hakimu aliahirisha kesi hizo hadi Julai 28,2022,huku akiagiza Julai 19,mwaka huu mshitakiwa huyo wa nne (Daniel) kupelekwa mahakamani hapo kwa ajili ya kukamilisha taratibu za dhamana.

 


0 Comments:

Post a Comment