Ajali ya Ambulansi na Guta Yaua Watu 7, Yajeruhi 15 Mjini Mafinga




Watu saba wamepoteza maisha na wengine 15 kujeruhiwa katika ajali mbaya iliyohusisha gari la kubebea wagonjwa (ambulance) na guta lililokuwa limebeba watu 22 waliokuwa wakielekea shambani. 

Ajali hiyo imetokea leo, Aprili 19, 2025, katika barabara ya Mafinga kuelekea Luganga, karibu na ofisi za Halmashauri ya Mji wa Mafinga, mkoani Iringa.

Kwa mujibu wa taarifa ya mashuhuda wa ajali hiyo, guta hilo lilikuwa limebeba watu wengi kupita uwezo wake, na lilipofika eneo la tukio, liligongana uso kwa uso na gari la wagonjwa aina ya Land Cruiser lenye namba za usajili STM 7840, ambalo lilikuwa linatoka Luganga.

Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dkt. Linda Salekwa, alipofika katika Hospitali ya Mji wa Mafinga alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza masikitiko yake kufuatia vifo hivyo.

"Watu hawa walikuwa wanakwenda shamba kwa kutumia usafiri ambao ni hatarishi kwao. Natoa wito kwa wananchi kuepuka kutumia vyombo vya usafiri visivyo salama ili kulinda maisha yao," amesema Dkt. Salekwa.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mji wa Mafinga, Dkt. Victor Msafiri, amethibitisha kupokea miili ya watu saba na majeruhi 15.

"Majira ya saa kumi na mbili asubuhi tumepokea majeruhi 15 na miili 7 ya marehemu wa ajali hii mbaya. Baadhi ya majeruhi wapo katika hali mahututi na wanaendelea kupatiwa matibabu," amesema Dkt. Msafiri.

Ajali hiyo imesababisha taharuki kwa wakazi wa Mafinga huku vyombo vya usalama vikiendelea na uchunguzi kubaini chanzo kamili cha ajali. 

Wakati huo huo, viongozi wa serikali wamewataka wananchi kuchukua tahadhari wanapotumia vyombo vya usafiri, hasa katika maeneo ya vijijini.

0 Comments:

Post a Comment