VIJANA SITA WASHITAKIWA KWA MPANGO WA KUMTEKA NA KUMLAWITI MFANYABIASHARA TARIMO



Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni imeelezwa kuwa vijana sita, wakiwemo mabondia wawili, walipanga kumteka mfanyabiashara Deogratus Tarimo kwa lengo la kumlawiti na kumsababishia maumivu.




Kesi hiyo imeendelea kusikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Ramadhani Rugemalira, ambapo washtakiwa Fredrick Nsato (21), bondia Isaack Mwaifuani (29), Benk Mwakalebela (40), bondia Bato Twelve (32), dereva teksi Nelson Msela (24), na Anitha Temba (27) maarufu kama Jack, wanakabiliwa na mashtaka ya utekaji nyara.


Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, amesema kuwa Anitha alihusika katika kumshawishi Tarimo kukutana naye hotelini kwa madai ya kujadili biashara. Hata hivyo, alipofika hotelini hapo, alinaswa kwenye mtego wa washitakiwa waliokuwa na mpango wa kumteka.


Ilidaiwa kuwa Novemba 11, 2024, Tarimo alipofika hotelini, Anitha alimwelekeza kusubiri katika kaunta ya baa. Baada ya muda mfupi, washtakiwa Mwaifuani, Mwakalebela, na Twelve waliwasili katika gari aina ya Toyota Raum namba T 237 EGE na kujitambulisha kama polisi.


Walipomvuta Tarimo kuelekea kwenye gari hilo, alipiga kelele, hali iliyowalazimu kumwachia na kumtishia kuwa wangempata tena. Taarifa zilifikishwa katika Kituo cha Polisi Gogoni, ambapo uchunguzi ulifanyika na hatimaye washitakiwa wakakamatwa.


Katika utetezi wao, washtakiwa wote walikana mashtaka dhidi yao, huku Anitha Temba akikataa jina lake maarufu la Jack. Mahakama ilikubali ombi la kubadilisha shtaka kutoka "jaribio la utekaji" hadi "utekaji nyara" baada ya ushahidi mpya kuwasilishwa.


Kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 24, 2025, kwa ajili ya kusikilizwa zaidi.

0 Comments:

Post a Comment