Mapacha Wakamatwa Kwa Tuhuma za Mauaji ya Mama Yao, Mkulima Aua Akigombea Nyama ya Kenge


Jeshi la Polisi Mkoani Mtwara limefanikiwa kuwakamata mapacha wawili, Danford Steven Seif (24) na Daniel Steven Seif (24), kwa tuhuma za kumuua mama yao, Upendo Methew Mayaya (42), ambaye ni mkazi wa Wilaya ya Masasi. 


Watuhumiwa hao walikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za mauaji yaliyotokea tarehe 15 Desemba 2024, baada ya kumshambulia mama yao kwa kutumia jembe na mwichi, na kumjeruhi vibaya katika paji la uso, majeraha yaliyosababisha kifo chake.



Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, SACP Issa Suleiman, alithibitisha tukio hili na kusema: "Watuhumiwa hao walitekeleza kitendo hicho tarehe 15 Desemba 2024 kwa kumpiga mama yao katika paji la uso kwa kutumia jembe na mwichi na kumsababishia majeraha yaliyopelekea kifo chake. Chanzo cha mauaji hayo ni imani za kishirikina."

Aidha, Jeshi la Polisi pia limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wengine wakiwa na dawa za kulevya na pombe haramu. Katika operesheni iliyofanyika kuanzia tarehe 1 hadi 31 Desemba 2024, polisi walikamata watuhumiwa 25 kwa tuhuma za mauaji, kulawiti, wizi, pombe haramu, na nyara za serikali.

Katika tukio lingine, Renard Godfrey Ndonjima (62), mkulima kutoka Kijiji cha Lilala Wilaya ya Masasi, alikamatwa kwa tuhuma za kumuua Mohamed Kapile (52), mkulima kutoka Kijiji cha Songambele Wilaya ya Nachingwea. Mauaji haya yalitokea tarehe 22 Desemba 2024, baada ya mtuhumiwa na marehemu kugombania nyama ya kenge. Kamanda Suleiman alisema: "Chanzo cha mauaji hayo ni mtuhumiwa na marehemu kugombania nyama ya kenge."


Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara linawashukuru wananchi kwa ushirikiano mkubwa waliouonesha mwaka 2024 katika kubaini na kutanzua uhalifu. Kamanda Suleiman alitoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Mtwara kuwa na umoja katika kuhakikisha ulinzi na usalama, akisema: "Jukumu la ulinzi na usalama wa nchi ni la kila mmoja wetu. Wanapona vitendo vya uhalifu, wasisite kutoa taarifa kwa wakati."

0 Comments:

Post a Comment