FUATA USHAURI HUU UMALIZE TATIZO LA MENO NA FIZI

 

"UKIAMKA asubuhi kunywa chai kisha kapige mswaki, tumia dakika tano mpaka kumi kusafisha meno na maeneo mengine ya mdomo kwa mswaki ambao ni mwembamba ili kuhakikisha maeneo yote ya mdomo yanafikiwa na mswaki,".

 

Hayo ni maneno ya Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel ambaye kitaaluma ni daktari wa binadamu aliyebobea kwenye tiba ya kinywa na meno ameyasema hayo leo, Julai 19, 2022  wakati alipotembelea kambi ya wiki moja inayoendeshwa na madaktari bingwa na wauguzi 25 wa kujitolea kutoka nchini Uingereza kwenye hospitali ya rufaa ya mkoa  wa Arusha, Mount Meru.

 

Amesema kuwa matatizo ya kinywa na meno yanachangiwa kwa kiasi kubwa na mtindo wa maisha ambapo watu wanakula vitu vya sukari, vileo na sigara  huku wakishindwa kufuata taratibu za kitaalam za kupiga mswaki.

 

"Ukiboresha afya ya kinywa na meno inawasaidia kuepukana na gharama baadaye ya kujitibu magonjwa mengine ikiwemo matatizo ya moyo,” alisema Dk Mollel akiongea mara baada ya kufika kwenye kambi hiyo ambayo kwa siku inahudumia wastani wa wagonjwa 80 na kuongeza.

 

…Tukiwa na utaratibu wa kufanya uchunguzi wa afya ya kinywa unaweza kugundua haraka sana tatizo la ugonjwa wa sukari kabla halijafika sehemu ambayo inaweza kukuletea shida.

 

“Ili jino litoboke au meno yapate shida inatakiwa kuwa na chakula na bakteria ambao wapo mdomoni siku zote huwezi kuwaondoa ila kuna kitu kinaitwa muda ambao chakula kitakaa mdomoni,”

 

Dk Mollel anasema kuwa  bakteria hao wana tabia ya kuozesha chakula kikikaa kwenye meno na wakishaozesha chakula wanatengeneza tindikali inayotoboa meno.

  

 Alisema kuwa uozeshaji huo wa chakula unatokea saa nane baada ya mtu kumaliza kula na kukaa bila kusafisha kinywa kwa maswaki.

 

" unachotakiwa kufanya unahakikisha usiku kabla ya kulala kunafisha kinywa chako kwa kupiga mswaki  vizuri manake usiku mzunguko wa mate mdomoni huwa ni mdogo na mate yanatabia ya kukulinda yakipungua bakteria wanafanya kazi kubwa ndani ya mdomo,” alisema Dk Mollel na kuongeza.

 

…Unachotakiwa kufanya unapiga mswaki vizuri, unalala na mdomo msafi ambao hauna chakula hivyo bakteria watakosa kitu cha kuchakata ili watengeneze tindikali au zile sumusumu,”.

 

“Ukiamka asubuhi mdomo wako si ulishausafisha kabla ya kulala hivyo ni msafi ukiamka moja kwa moja unakunywa chai baada ya hapo unapiga mswaki ndiyo unaenda zako kazini,”.

 

Hata hivyo Naibu Waziri huyo wa Afya ameshauri ni vizuri kumuona daktari wa meno walau mara mbili kwa mwaka ili kufanyiwa uchunguzi wa kinywa na meno.

 

Awali Dk Mollel mara baada ya kutembelea kambi hiyo aliwapongeza na kuwashukuru madaktari hao wa kujitolea kutoka nchini Uingereza wa taasisi ya Smile Star,  pamoja na mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo kupitia taasisi yake ya Alama Afrika na kampuni ya usafirishaji wa mizigo ya jijini Arusha ya AVCO ambao kwa pamoja wameshirikiana kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa mafanikio.

 

"Kimsingi huduma ambayo mnaitoa ilitakiwa serikali itafute fedha na vifaa ninavyoviona hapa leo ambavyo mnawagaia Watanzania bure ina maana serikali ilikuwa iingie gharama hiyo lakini nyie mmeibebaba asanteni sana sasa serikali itatumia fedha hizo kuhudumia wananchi kwenye eneo jingine ,"ameshukuru Dk Mollel.

 

Kwa upande wake, kiongozi wa msafara huo kutoka Uingereza, Dk Mitesh Badian amesema kuwa wametumia paundi za Uingereza 80,000 ambazo ni sawa na zaidi ya shilingi 230,000 milioni za Tanzania kugharamia vifaa tiba na kuja nchini pamoja na msafara huo wenye madaktari bingwa na wauguzi wa afya ya kinywa na meno 25.

  

"Mimi nimezaliwa Kisumu (Kenya) hata kama nimekaa ulaya miaka 40 lakini ndani ya mioyo yetu mimi na wenzangu sisi ni waafrika hivyo tunana tuna wajibu wa kuwasaidia watu wetu,” amesema Dk Mitesh na kuongeza. 

 

…Hii ni safari ya 22 nimekuja kutoa huduma Afrika  na ni mara ya pili kuja Tanzania kwani mara ya kwanza tulifanya kambi kama hii Mufindi mwaka 2013,”.

 

“Hii imewezekana pia kutokana na moyo wa kujitolea wa madaktari bingwa na wauguzi ambao hawapati chochote kutoka na kazi hii wanayofanya hapa na tunajipanga mpango huu uwe endelevu tuwe tunakuja kila mwaka,”.

 

Hata hivyo Dk Mitesh ameshauri uanzishwe  mpango wa kutoa elimu ya afya ya kinywa kwa vitendo kwa wanafunzi ili kuweza kuilinda jamii na magonjwa ya kinywa ambayo yanamadhara makubwa yasipodhibitiwa mapema.

 

Amesema kuwa mpango huo utaonyesha matokeo makubwa kwa jamii ingawa alionya matokeo hayo hayawezi kuonekana ndani ya muda mfupi kwani inaweza kuchukua mpaka miaka 20 kukamilika lakini utasaidia kumaliza matatizo ya meno na fizi.

 

Naye Dk Pip ambaye pia anamiliki kliniki ya meno ya Smile Star nchini Uingereza amesema kuwa wanatarajia kuwa wanakuja Tanzania kila mwaka mwezi Mei kwa ajili ya kutoa huduma kama hiyo ambapo mbali ya hapo kwenye hospitali ya mkoa wanatazamia kufika kwenye maeneo ya  vijijini.


Hata hivyo amesema kuwa changamoto wanayoiona ni kupata maeneo salama kwa ajili ya kuweka kambi na kutoa huduma hiyo ambapo wanadhani huko kutakuwa na wagonjwa wengi kwani kwa Arusha Mjini ambapo kuna hospitali kubwa na ndogo nyingi kwa  siku moja wamekuwa wakitoa huduma ya wastani wa wagonjwa zaidi ya 80 tokea waanze kambi hiyo Julai 18, mwaka huu itakayodumu kwa wiki moja.

 

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kampuni ya Usafirishaji ya AVCO, Kakea Dhariwal ambaye ni miongoni mwa waliochangia ujio wa wataalam hao amewashukuru wataalam hao kutoka Uingereza akiwemo mdogo wake  Dk Pip ambaye alisoma jijini Arusha kwenye  shule ya kimataifa ya Arusha Meru kabla ya kuhamia nchini Uingereza mwaka 1982.

 

"Amefanya bidii sana,  kule anafanya biashara sasa yeye na marafiki zake kama mnavyoona wanaongea kiswahili kwa kuwa wametoka huku kwetu kwa sababu mioyo yao iko Afrika na wanarudi Afrika kusaidia," amesema Kakea.

 

Ameweka msisitizo kwenye umuhimu wa kutoa elimu ya afya na kinywa mashuleni ambapo alisema kuwa program hiyo inaweza kusaidiwa kupata vifaa vya kufundishia kwa vityendo ikiwemo miswaki, dawa za meno na picha mbalimbali kutoka kwa wataalam hao wa Uingereza.

 

Kwa upande wake, mwananchi kutoka kata ya Elerai jijini Arusha, Nasib Seleman aliwashukuru madaktari hao kwa kumpatia tiba ya fizi zake zilizokuwa zikimuuma pamoja na kumng'oa jino lake lililokuwa limeharibika.

 

" Huduma yao ni nzuri sana na ni wakarimu, wanaonyesha ukarimu kwa watu kama sisi ambao hatuna uwezo wa kushughulikia matatizo kama haya kwa haraka,” anasema Nasib na kuongeza.

 

…Niliwahi kung'oa jino hospitali ya Kaloleni huduma ilikuwa nzuri ila hawa wenzetu (madaktari wa Uingereza) wako vizuri zaidi kwa sababu unapong'oa jino lazima utasikia maumivu makali kwa huku kwetu lakini hapa (kwenye kambi hiyo maalum)  unang'olewa jino na unakuwa uko vizuri tu unanyanyuka unaondoka,".

 

Naye, Daktari bingwa wa afya ya kinywa na meno kutoka hospitali ya rufaa ya mkoa wa Arusha, Dk Thadei Mosha, amesema kuwa matatizo ya kinywa na meno bado ni changamoto kubwa nchini hasa kutoboka kwa meno na maumivu ya fizi ambayo kwa kiasi kikubwa yanasababishwa na kutokupiga mswaki vizuri.

 

"Kwenye kinywa cha binadamu kuna vimelea bakteria ambao wapo mdomoni na hawa bakteria wakitengenezewa mazingira ya uchafu basi wakikutana na sukari wanatengeneza tindikali inayopelekea meno kutoboka,” amefafanua zaidi Dk Mosha na kuongeza.

 

…Lakini pia bakteria hao wakikaa muda mrefu kwenye maeneo kuzunguka fizi wanaleta magonjwa ya fizi ambayo mara nyingi hayana maumivu ila dalili kubwa ni fizi kuvimba, kutoa damu na harufu mbaya ya kunywa lakini baadaye meno yanalegea na kutoka,”. 

 

“Watu wengi wenye umri mkubwa wanasema hawajui imekuwaje wanaona meno yanalegea na kutoka ila tatizo kubwa hawajui kutunza meno yao na hawafiki kwa wataalam wa kinywa na meno kwa wakati basi wanaishia kupata shida,”.

 

“Kama unavyojua wataalam wa kinywa na meno nchini bado si wengi hivyo tunapopata wataalam kama hawa (kutoka Uingereza) basi wanatusaidia kupunguza shida kwa watu wengi kwa kiasi kikubwa,”. 

 

Dk Mosha amesema kuwa kwa kawaida hospitalini hapo kwa siku hupokea wagonjwa wa kinywa na meno si chini ya 20 jambo alilodai kuwa linaonyesha ni kiasi gani tatizo hili ni kubwa na kwa  Julai 18,mwaka   wataalam hao kutoka Uingereza  wameweza kuwaona na kuwatibu wagonjwa zaidi ya 80 waliokuwa na shida ya kinywa na meno 

 

Shida kwenye jamii ni kubwa na tutaendelea kushirikiana na wadau kutoka nje wakati mwingine kuendesha kambi kama hizi hata sisi mwezi wa tatu wakati wa wiki ya kinywa na meno tuliweka kambi sawa na hii kabisa kuhudumia wagonjwa zaidi ya 1,000 ndani ya siku 

0 Comments:

Post a Comment