Aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Simanjiro Afikishwa Mahakamani kwa Matumizi Mabaya ya Madaraka



Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Samweli Warioba Gunzar, amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara kwa makosa mawili ya matumizi mabaya ya madaraka na kutotimiza wajibu wa kisheria, hatua inayokiuka sheria.


Akisoma shauri hilo, Mwendesha Mashtaka wa Takukuru Wilaya ya Simanjiro, Wakili Faustin Mushi, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu na Mfawidhi wa Wilaya ya Simanjiro, Charles Uisso, alisema kuwa mshitakiwa, akiwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, alitoa zabuni ya ukusanyaji wa mapato ya soko la mnada wa Orkesumet kwa mwananchi aitwaye Elias Lazaro Tipiliti, bila ya kuwepo kwa tangazo la zabuni na bila ya zabuni hiyo kushindanishwa.


"Mshitakiwa alitoa zabuni kwa Elias Lazaro Tipiliti bila kufuata taratibu za kisheria, jambo ambalo ni kinyume cha sheria," alisema Mwendesha Mashtaka, Faustin Mushi.


Aidha, Mwendesha Mashtaka huyo aliongeza kuwa mshitakiwa amekana makosa yote mawili na kwamba yupo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana kwa kupeleka wadhamini wawili ambao ni watumishi wa umma, pamoja na kusaini bondi ya shilingi milioni mbili.


"Kesi hii imepangwa kusikilizwa tena Februari 11 mwaka huu, kwa ajili ya kusikilizwa kwa mashahidi wa upande wa Jamhuri," alisisitiza Wakili Mushi.

0 Comments:

Post a Comment