Arusha Mjini Maandalizi ya Uchaguzi Yamekamilika kwa Asilimia 100, Usalama Waimarishwa



Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini, Joseph Mkude, amesema kuwa maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 katika Jiji la Arusha yamekamilika kwa asilimia 100, huku akisisitiza kuwa hali ya usalama na amani imeimarishwa kikamilifu ili kuhakikisha wananchi wanashiriki uchaguzi huo kwa utulivu na haki.



Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Arusha, Mhe. Mkude alisema kuwa wananchi hawapaswi kuwa na hofu yoyote, kwani vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga vyema kuhakikisha zoezi la upigaji kura linakwenda vizuri na bila vurugu.

“Tuna jumla ya mitaa 154 na vituo 1,051 vya kupigia kura. Tumeongeza idadi ya vituo ili kurahisisha upigaji kura na kuhakikisha kila Mtanzania anapata nafasi ya kutimiza haki yake ya kikatiba bila kutembea umbali mrefu,” alisema Mkude.

Ameongeza kuwa serikali imeweka mikakati madhubuti ya kudumisha amani na kuwataka wananchi waende kupiga kura kwa utulivu kisha kurejea majumbani mwao au kuendelea na shughuli zao za kila siku.

“Baada ya kupiga kura, nendeni nyumbani au endeleeni na shughuli zenu. Jioni msikilize matokeo kupitia vyombo vya habari rasmi. Tusiwe na mikusanyiko isiyo na maana, kwani amani ndiyo msingi wa maendeleo yetu,” alisisitiza Mkude.

Aidha, ametoa wito kwa vijana kuachana na kauli za uchochezi dhidi ya Serikali au Tume ya Uchaguzi, akiwataka watambue kuwa amani ni nguzo muhimu katika kuijenga Tanzania.

“Hatutegemei kuwa na maandamano yoyote, kwa sababu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alishasisitiza kuwa maandamano pekee yanayokubalika ni ya kwenda kupiga kura na si vinginevyo,” alisema Mkude.

Kwa mujibu wa Mkude, hadi sasa hakuna chama chochote cha siasa kilicholalamika kufanyiwa vitendo vya ukiukwaji wa sheria wakati wa kampeni, huku akibainisha kuwa vyama vyote vimefanya kampeni zao kwa amani na kufuata sheria.

“Vifaa vyote vya uchaguzi vimewasili salama, miundombinu ipo vizuri, na usalama umeimarishwa vya kutosha. Wananchi wasiwe na wasiwasi, wajitokeze kwa wingi tarehe 29 Oktoba 2025 kupiga kura,” alisema Mkude.

Amebainisha kuwa jumla ya wapiga kura 435,000 wanatarajiwa kushiriki katika uchaguzi huo ndani ya Jiji la Arusha.

Pia, aliwahakikishia wafanyabiashara kuwa shughuli za kiuchumi zitaendelea kama kawaida siku ya uchaguzi, kwani ulinzi utakuwepo wa kutosha katika maeneo yote ya jiji hilo.

“Sisi kazi yetu ni kulinda raia na mali zao. Wafanyabiashara wasiwe na hofu, baada ya kupiga kura wanaweza kufungua biashara zao kama kawaida, ulinzi upo wa kutosha,” alisema Mkude.


0 Comments:

Post a Comment