Makuyuni Wildlife Park Yaendelea Kung’ara Katika Ramani ya Utalii wa Kimataifa





Hifadhi ya Makuyuni Wildlife Park, iliyopo wilayani Monduli mkoani Arusha chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), inaendelea kujitokeza kama lulu mpya ya utalii wa kanda ya kaskazini, kwa kuvutia wageni wa ndani na nje ya nchi kutokana na mandhari yake ya asili na utajiri wa wanyamapori wa aina mbalimbali.



Tarehe 8 Septemba 2025, hifadhi hiyo ilipokea kundi la wageni wa kimataifa kutoka mataifa ya Denmark, Australia na New Zealand waliowasili kupitia kampuni maarufu ya utalii, Ranger Safaris & Tours yenye makao yake makuu jijini Arusha.



Wageni hao zaidi ya ishirini walitembelea hifadhi hiyo na kueleza kuridhishwa kwao na ubora wa huduma, mazingira ya hifadhi na uzoefu wa kipekee walioupata katika safari yao. Baadhi yao walionesha nia ya kurejea tena mwezi Novemba kwa ziara ya pili.

Aidha, wageni hao wameahidi kusaidia kuitangaza Makuyuni Wildlife Park kupitia mitandao yao ya kijamii na majukwaa ya utalii katika nchi walizotoka, hatua inayotarajiwa kuongeza umaarufu wa hifadhi hiyo katika masoko ya kimataifa.



Makuyuni Wildlife Park ni moja ya hifadhi mpya zinazokua kwa kasi nchini, ikiwa na fursa kubwa za kukuza utalii endelevu. Kupitia juhudi za TAWA, hifadhi hii imeboreshwa kwa kujengewa miundombinu rafiki kwa watalii na kulindwa kwa viwango vya kitaifa, jambo linaloifanya kuwa kivutio kipya chenye hadhi ya kimataifa.

Kwa mujibu wa maelezo kutoka kwa maafisa wa TAWA, hifadhi hiyo inaendelea kupata wageni kutoka nchi mbalimbali na kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi katika eneo la Makuyuni na viunga vyake.


0 Comments:

Post a Comment