Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, amekutana na Balozi mpya wa Tanzania nchini Japan, Anderson Mutatembwa, na kumwelekeza kuhakikisha anatekeleza kwa vitendo sera ya mambo ya nje kwa kuimarisha diplomasia ya uchumi, kuvutia wawekezaji, kutangaza vivutio vya utalii, na kukuza matumizi ya lugha ya Kiswahili nchini humo.
Akizungumza ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma leo, Septemba 8, 2025, Waziri Mkuu alisema:
"Ni jukumu lako kwenda kutangaza fursa zilizopo hapa nchini, tumia vizuri mahusiano yetu na Japan kupata wawekezaji katika maeneo mbalimbali. Zipo fursa nyingi ambazo tunahitaji kuzipata hasa za kiuchumi, ukifika huko weka mpango wa kutembelea wawekezaji, yapo maeneo ambayo tunahitaji kunufaika."
Katika mazungumzo hayo, Waziri Mkuu alisisitiza umuhimu wa kutumia uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Japan kama jukwaa la kukuza uchumi wa taifa. Alimtaka Balozi Mutatembwa kuhakikisha anawatembelea wawekezaji nchini Japan na kuwaeleza kuhusu mazingira bora ya uwekezaji yaliyopo Tanzania.
Pia alimtaka balozi huyo kuendeleza jitihada za kuwaunganisha Watanzania wanaoishi nchini Japan ili washiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.
"Weka mpango wa kuwaunganisha Watanzania waishio nchini Japan na kuwahamasisha kushiriki katika fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo nchini humo jambo ambalo litaiwezesha Tanzania kunufaika na hatua hizo."
Waziri Mkuu pia alisisitiza umuhimu wa kuitangaza Tanzania kama kivutio cha utalii, akieleza kuwa masoko ya utalii kutoka Japan yanaweza kuongeza mchango mkubwa katika pato la taifa:
"Tumia majukwaa mbalimbali kuhamasisha Wajapan kuja kuitembelea Tanzania. Lengo letu ni kuhakikisha tunaongeza idadi ya watalii nchini."
Katika nyanja ya lugha na utamaduni, Waziri Mkuu alihimiza juhudi za kuitangaza lugha ya Kiswahili nchini Japan:
"Ukiwa huko jitahidi kupanua wigo wa matumizi ya lugha ya Kiswahili."
Mkutano huo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha kwamba balozi mpya anaanza majukumu yake kwa mwelekeo sahihi unaoendana na vipaumbele vya kitaifa hususan katika maeneo ya uchumi, utalii, lugha na ushirikiano wa kimataifa.
0 Comments:
Post a Comment