ARUSHA, TANZANIA –Mkutano wa Pili wa Baraza la Vyombo Huru vya Habari Afrika (Pan-African Media Summit 2025) umefunguliwa rasmi jijini Arusha, ambapo viongozi waandamizi kutoka mashirika ya kimataifa, taasisi za serikali, mabaraza ya habari na wanahabari kutoka kote barani Afrika wameweka msisitizo juu ya umuhimu wa kujenga mazingira wezeshi yanayochochea uandishi wa habari wa kitaaluma, kimaadili na huru.
Mgeni rasmi katika mkutano huo, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mawasiliano na Habari wa UNESCO makao makuu, Paris – Ufaransa, Dkt. Tawfik Jelassi, alihimiza kuimarishwa kwa mifumo ya kisheria, sera, na kanuni ambazo zitasaidia sekta ya habari kukabiliana na changamoto za kisasa ikiwa ni pamoja na teknolojia, taarifa potofu na akili mnemba (AI).
“Tunapokutana leo hapa Arusha, dunia nzima inakabiliwa na mabadiliko makubwa. Imani ya watu kwa vyombo vya habari inapimwa, teknolojia inabadilisha namna taarifa zinavyoundwa na kusambazwa, huku uhuru wa kujieleza ukikumbwa na mashinikizo duniani kote,” alisema Dkt. Jelassi.
Akinukuu Azimio la Windhoek la mwaka 1991, ambalo lilitokana na Mkutano wa Uhuru wa Vyombo vya Habari duniani ulioandaliwa na UNESCO, Dkt. Jelassi alikumbusha:
“Azimio linasema: ‘Kuanzishwa, kudumishwa na kuendelezwa kwa vyombo vya habari huru, vya watu wengi na visivyoegemea upande wowote ni jambo la lazima kwa maendeleo na ustawi wa demokrasia.’ Hii ni dira iliyoanzishwa Afrika, na leo bado ina umuhimu mkubwa kuliko wakati wowote.”
Aidha, Dkt. Jelassi aliwasilisha rasmi waraka wa UNESCO uitwao “UNESCO Guidelines for the Governance of Digital Platforms”, akisema:
“Mwongozo huu ni matokeo ya kazi ya miaka miwili iliyohusisha nchi wanachama 194 wa UNESCO, mashirika ya kiraia, vyombo vya habari, makampuni ya teknolojia, taasisi za elimu na wataalamu wa sekta. Unalenga kuhakikisha kuwa majukwaa ya kidijitali yanakuwa wazi, yanawajibika na yanaheshimu uhuru wa kujieleza.”
Kwa mujibu wa Dkt. Jelassi, udhibiti wa vyombo vya habari na majukwaa ya kidijitali lazima uwe shirikishi na ujumuishi:“Udhibiti bora lazima ujumuishwe tangu awali. Unapaswa kuzingatia usawa wa kijinsia, haki za watu wenye ulemavu na kulinda sauti za makundi yaliyoko pembezoni.”
Serikali ya Tanzania: Tumeanza Mageuzi ya Kisheria
Awali, akimkaribisha mgeni rasmi, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO, Rodney Mbuya, alisema mkutano huo ni muhimu kwa kuwa unajadili kwa kina mustakabali wa sekta ya habari barani Afrika, na pia unawapa serikali fursa ya kujifunza kutoka kwa wengine.
“Tanzania tayari imeanza kufanya maboresho ya kisheria, hususan Sheria ya Huduma za Habari (Sura 229), ambapo vipengele mbalimbali vimebadilishwa ili kuboresha mazingira ya kazi kwa waandishi wa habari,” alisema Mbuya.
Aliongeza kuwa sasa kuna 'Bodi ya Ithibati' inayosimamia uhalali wa wanahabari nchini:
“Lengo ni kuhakikisha sekta hii inajengwa kwa msingi wa taaluma, siyo kila mtu kuingia bila sifa. Takribani waandishi 3,000 tayari wameomba usajili, na wengi wao wameshapata vyeti vyao.”
“Tunaamini sasa tutashuhudia mabadiliko makubwa. Uandishi wa habari utaandikwa kwa weledi na kwa kufuata maadili, kwa sababu wanaofanya kazi hiyo ni wale waliopitia mafunzo rasmi,” alisisitiza.
MCT: Tujenge Ushirikiano wa Bara Zima
Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), **Ernest Sungura**, akitoa hotuba ya ufunguzi wa mkutano, alisisitiza umuhimu wa kuunganisha nguvu ya mabaraza ya habari barani Afrika kwa ajili ya kulinda uhuru wa vyombo vya habari na kukuza weledi wa wanahabari.
“Huu si mkutano wa kawaida. Ni fursa ya kihistoria ya kuimarisha ushirikiano wa mabaraza ya habari Afrika ili kusukuma mbele mapinduzi ya sekta hii kwa ubunifu na mshikamano,” alisema Sungura.
“Tunasimama pamoja kuthibitisha dhamira yetu ya kulinda uhuru wa vyombo vya habari, kuinua viwango vya maadili, na kuunda simulizi ya Kiafrika yenye nguvu, ushujaa na uhalisia.”
Akikumbusha historia ya MCT, Sungura alitangaza:“Baraza la Habari Tanzania linatimiza miaka 30 ya kujisimamia. Tutaadhimisha mafanikio haya leo jioni, tukitafakari tulikotoka na kuangalia mbele kwa matumaini.”q
Pia, aliwapongeza wadhamini waliowezesha kufanikisha mkutano huo akiwemo UNESCO, TAIFA GAS, AZAM Media, TANAPA, TRA, NCAA, WCF, PSSSF, TPA, NMB Bank, na wengine: “Tunawashukuru kwa dhati kwa msaada wenu mkubwa. Ushirikiano wenu ndiyo nguzo ya mafanikio haya,” alisema.
Mkutano huu umeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Network of Independent Media Councils of Africa (NIMCA), Media Council of Tanzania (MCT) na East Africa Press Councils (EAPC) na unafanyika sambamba na MC\&T Expo, maonesho ya teknolojia, huduma na uvumbuzi unaobadilisha mazingira ya habari barani Afrika.
“Kupitia MC\&T Expo, tunalenga kuonesha mustakabali wa kidijitali wa Afrika, kuhamasisha ubunifu na kuunganisha wadau wanaoleta mabadiliko,” alihitimisha Sungura.
Mkutano wa Pan-African Media Summit 2025 unaendelea kwa siku mbili jijini Arusha, ukiwa na lengo kuu la kuimarisha weledi wa uandishi wa habari, uhuru wa kujieleza, na usimamizi jumuishi wa mawasiliano katika enzi ya mabadiliko ya kidijitali.







0 Comments:
Post a Comment