KESI ya unyang'anyi wa kutumia silaha inayomkabili aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili sasa kusikilizwa kwa wiki mbili mfululizo kwenye mahakama ya hakimu mkazi Arusha baada ya kesi ya awali iliyokuwa kwenye mahakama ya wilaya ya Arusha kufutwa.
Aidha upande wa Jamhuri unatazamia kuleta mashahidi 10 na vielelezo 10 kwenye shauri hilo la jinai namba 105/2021 ambapo washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka matatu ya unyanganyi wa kutumia baada ya lile la awali namba 66/2021 kufutwa kutokana na maombi ya mawakili wa serikali.
Shauri hilo linasikilizwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Odira Amworo, ambapo upande wa serikali unawakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu Tumaini Kweka,Wakili wa serikali mwandamizi, Abdallah Chavula na Wakili wa serikali Baraka Mgaya huku washitakiwa wakitetewa na mawakili Moses Mahuna na Dancan Oola.
Washitakiwa wengine katika shauri hilo ni Sylvester Nyegu na Daniel Mbura,
Wakili Chavula amewasomea mashitaka yao ambapo katika kosa la kwanza la unyang’anyi wa kutumia silaha linalowakabili washitakiwa wote watatu amedai kuwa mnamo Februari 9,2021 katika Mtaa wa Bondeni jijini Arusha washitakiwa wote kwa pamoja waliiba Sh Milioni 2.76 mali ya Mohamed Saad.
Alidai kuwa kabla ya kufanya wizi huo waliwashambulia Numan Jasini, Harijin saad Harijin, Bakari Msangi, Salim Hassan na Ally Shaban kwa kuwapiga na walitumia silaha aina ya bunduki kuwatisha.
Katika shitaka la pili la wizi wa kutumia silaha, washitakiwa hao wanadaiwa kuwa siki hiyohiyo waliiba fedha Sh 390,000 mali ya Bakari Msangi ambaye ni Diwani wa Kata ya Sombetini na kabla ya kufanya tukio hilo walimfunga pingu, kumpiga na kumshambulia huku akimtishia na bunduki.
Shitaka la tatu linalowakabili washitakiwa wote pia ni wizi wa kutumia silaha ambapo wanadaiwa katika mtaa huo waliiba Sh 35,000 na simu ya mkononi aina ya Tecno mali ya Ramadhan Rashid na kuwa baada ya wizi huo walimfunga pingu, kumpiga na kumtisha kwa bastola.
Washitakiwa walikana mashitaka yote ambapo wakili wa serikali Chavula aliwasomea hoja za awali ambapo alidai washitakiwa wote watatu walifika katika duka linalomilikiwa na Mohamed Saad ambapo mshitakiwa, Sabaya alijitambulisha kama Mkuu wa wilaya ya Hai na kutaka kujua alipo mmiliki wa duka hilo huku akiwaweka chini ya ulinzi watu aliowakuta dukani hapo.
Alidai mbali ya kuiba fedha hizo Sh Milioni 2.76 ambazo zilikuwa za mauzo,simu na Sh 390,000 mali ya Msangi na Sh 35,000 mali ya Rashid,watuhumiwa hao walipekua eneo la kaunta na kuchukua mashine mbili za EFD’s na kuondoka nazo.
“Washitakiwa hawakuishia hapo pia walipekua eneo la kaunta na wakachukua mashine za kiektroniki zinazotumika kutolea risiti (EFD’s) na kuiba fedha hizo za mauzo na waliendelea kuwapiga watu hao waliokuwa ndani ya duka hilo na kuondoka wakiwa na mali walizoziiba,” Chavula aliieleza mahakama.
Washitakiwa walikana maelezo hayo ya hoja za awali ambapo hakimu, Amworo ameahirisha shauri hilo mpaka
Julai 19 mwaka huu litskaposikilizwa mfululizo mpaka Julai 30 mwaka huu baada ya wakili wa Serikali Mkuu, Kweka kuiomba mahakama kesi hiyo isikilizwe mfululizo.
KESI YA UHUJUMU UCHUMI
Kesi ya uhujumu uchumi namba 27/2021 inayomkabili Ole Sabaya na wenzake sita, imefika hatua za mwisho za upelelezi.
Wakili wa Serikali Mkuu Kweka,ameieleza mahakama ya wilaya ya Arusha mbele ya Hakimu, Martha Mahumbuga, anayesikiliza shauri hilo.
Aliiomba mahakama kuahirisha kesi hiyo mpaka tarehe nyingine aliyodai kuwa watatoa mwelekeo wa upelelezi siku shauri hilo litakapotudi mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa.
"Kesi ilipangwa leo kwa ajili ya kutajwa na kutoa mwenendo wa upelelezi,tumefikia hatua za mwisho za upelelezi na tunaomna tarehe nyingine ambapo tutatia mwelekeo wa upelelezi pia,"
Wakili wa utetezi Oola,aliieleza mahakama kuwa hawana pingamizi na irekodiwe kuwa wako kwenye hatua za mwisho za upelelezi.
Shauri hilo limeahirishwa hadi Julai 30,2021 itakaporudi mahakamani hapo kwa ajili ya kitajwa.

0 Comments:
Post a Comment