RAIS WA ZAMANI WA NIGERIA, BUHARI, KUZIKWA LEO

 


Rais wa zamani wa Nigeria, Muhammadu Buhari, anatarajiwa kuzikwa leo katika mji wa Daura, jimbo la Katsina, kaskazini-magharibi mwa Nigeria, baada ya kufariki dunia Jumatano katika hospitali moja mjini London alipokuwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa ambao haukujulikana. Buhari alikuwa na umri wa miaka 82.


Kifo chake kimethibitishwa rasmi na msemaji wa Ikulu ya Rais ambaye alieleza kuwa Buhari alifariki dunia saa 10:30 jioni kwa saa za London, na kwamba makamu wa rais Kashim Shettima pamoja na Mkuu wa Utumishi wa Ikulu wameelekea Uingereza ili kuusafirisha mwili wake kurudishwa nyumbani kwa maziko.



Akizungumza mara baada ya taarifa hiyo kusambaa, Rais wa sasa wa Nigeria, Bola Tinubu, ametangaza siku saba za maombolezo ya kitaifa kuanzia Julai 13. Katika kipindi hicho, bendera zote za taifa zitapepea nusu mlingoti kote nchini kama ishara ya heshima kwa kiongozi huyo wa zamani.


“Kama ishara ya heshima kwa kiongozi wetu wa zamani, nimeagiza kwamba bendera zote za kitaifa zipepee nusu mlingoti kote nchini kwa siku saba kuanzia leo,” alisema Rais Tinubu. “Serikali ya Shirikisho itampa Rais Buhari heshima kamili za serikali zinazostahili michango yake mikubwa kwa nchi yetu.”


Aidha, Rais Tinubu ametangaza kuitisha kikao cha dharura cha Baraza Kuu la Shirikisho Jumanne, Julai 15, kwa ajili ya kutoa heshima za kitaifa kwa marehemu Buhari.


Muhammadu Buhari alikuwa kiongozi mwenye historia ndefu ya utumishi kwa taifa. Alizaliwa mnamo Desemba 17, 1942 katika mji wa Daura. Aliongoza Nigeria mara mbili — kwanza kama kiongozi wa kijeshi baada ya mapinduzi ya mwaka 1983 hadi alipoondolewa madarakani mwaka 1985, kisha kama Rais aliyechaguliwa kidemokrasia kutoka mwaka 2015 hadi 2023.


Katika kipindi chake cha uongozi, Buhari alijitahidi kupambana na rushwa, ugaidi kutoka kwa kundi la Boko Haram, na kutekeleza mageuzi ya kiuchumi. Hata hivyo, serikali yake pia ilikumbwa na ukosoaji kuhusu hali ya usalama, uhuru wa vyombo vya habari, na changamoto za kiuchumi zilizoathiri maisha ya wananchi.


Rais Tinubu alimtaja Buhari kuwa “mwanajeshi, mzalendo na kiongozi wa kitaifa ambaye urithi wake wa utumishi na kujitolea utaendelea kukumbukwa.” Aliongeza kuwa, “alikuwa mtu mwenye msimamo, aliyekuwa tayari kufanya maamuzi magumu kwa ajili ya ustawi wa nchi yetu.”


Maziko ya Muhammadu Buhari yanatarajiwa kufanywa kwa mujibu wa taratibu za Kiislamu, huku viongozi wa ndani na wa kimataifa wakitoa rambirambi zao na kumuenzi kiongozi huyo aliyeacha alama kubwa katika historia ya Nigeria.


Kwa sasa, taifa linaendelea kuomboleza kifo cha mmoja wa viongozi wake waliotumikia kwa muda mrefu, huku watu mbalimbali wakimkumbuka kwa maamuzi yake, msimamo wake thabiti, na maono yake ya kuijenga Nigeria iliyo thabiti na yenye nidhamu.

0 Comments:

Post a Comment