TANAPA Yaendelea Kuboresha Vituo vya Malikale na Kuimarisha Utalii wa Kitamaduni



Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), CPA (T) Musa Nassoro Kuji, amesema kuwa TANAPA inaendelea kuboresha na kuimarisha vituo vya malikale ili kukuza utalii wa kitamaduni, ambao ni sehemu muhimu ya urithi wa Taifa.



Akizungumza katika kikao maalum na Mtwa Adam II Abdu Adam Sapi Mkwawa, Chifu wa Sita wa ukoo wa Mtwa Mkwawa (Kabila la Wahehe), Kamishna Kuji alibainisha kuwa vituo vya kihistoria vilivyokabidhiwa kwa TANAPA—ikiwemo Kituo cha Zana za Mawe Isimila na Makumbusho ya Mtwa Mkwawa—vimekuwa na mchango mkubwa katika kuvutia watalii na kuongeza pato la Taifa.


Kamishna Kuji alifanya ziara hiyo katika Makumbusho ya Mtwa Mkwawa, yaliyopo Kalenga, mkoani Iringa, ambako alisisitiza dhamira ya TANAPA kuhakikisha historia na utamaduni wa Watanzania unaendelezwa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

“Nakupongeza Mtwa Abdu Adam Sapi Mkwawa kwa juhudi zako katika kuhifadhi historia ya kabila la Wahehe na kumuenzi shujaa wetu Mtwa Mkwawa Mkwavinyika. Ushirikiano wenu na TANAPA pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii umechangia mafanikio makubwa, ikiwemo ushindi wa tuzo ya Hifadhi Bora Barani Afrika kupitia ‘World Travel Awards’ kwa upande wa vivutio vya kitamaduni,” alisema Kamishna Kuji.

Aliongeza kuwa TANAPA itaendelea kufanya maboresho ya miundombinu katika vituo hivyo vya kihistoria, kuhakikisha mandhari ya malikale na kumbukumbu za kihistoria zinalindwa ipasavyo na kubaki kuwa sehemu ya kivutio cha utalii endelevu.





Kwa upande wake, Mtwa Abdu Adam Sapi Mkwawa alimshukuru Kamishna Kuji kwa kutembelea makumbusho hayo, akieleza kuwa ziara hiyo ni ishara ya dhamira njema ya serikali na TANAPA katika kuimarisha historia ya Mtwa Mkwawa na kuifanya kuwa sehemu ya utambulisho wa Taifa.

“Tunashukuru sana kwa ujio wako. Tunaupokea kwa furaha kubwa na tunaamini ziara hii italeta matokeo chanya, ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa makumbusho haya ambayo ni nyenzo muhimu ya historia ya taifa letu,” alisema Mtwa Mkwawa.

Awali, Afisa Uhifadhi Mkuu Neema Mbwana, ambaye ni Mratibu wa Malikale zilizo chini ya TANAPA, alieleza kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025 kumekuwa na mafanikio makubwa. Aliyataja baadhi kuwa ni:

  • Utambuzi na uthamini wa vivutio vya malikale vilivyopo ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha na maeneo jirani,

  • Uandishi wa andiko la kimkakati kwa ajili ya uboreshaji wa vivutio hivyo,

  • Ukarabati wa miundombinu na majengo ya kihistoria,

  • Kuendeleza tafiti na kuimarisha ushirikishwaji wa jamii zinazozunguka vituo hivyo.


TANAPA inaendelea kutekeleza jukumu lake la kulinda na kuendeleza rasilimali za taifa, ikiwa ni pamoja na historia na utamaduni wa makabila ya Tanzania. Vituo vya kihistoria kama Kalenga na Isimila si tu vinabeba hadithi ya Taifa, bali pia vinatoa fursa ya kipekee kwa utalii wa kiutamaduni na kielimu.


0 Comments:

Post a Comment