JIJINI Nairobi, hali ya tahadhari imeshika kasi leo hii tarehe 7 Julai 2025, siku ya kumbukumbu ya Saba Saba, huku barabara zote kuu zinazoelekea jijini zikifungwa na idadi kubwa ya maafisa wa polisi wakionekana wakishika doria maeneo mbalimbali.
Hatua hii imechukuliwa na serikali ili kudhibiti maandamano yaliyopangwa na makundi mbalimbali ya kijamii na kisiasa kushinikiza mabadiliko ya kisera na haki za kijamii.
Kwa mujibu wa ripoti kutoka Nairobi Metropolitan Services, vizuizi vya barabarani vimewekwa katika maeneo mengi ya kuingia jiji, na magari ya usafiri wa umma yamezuiwa kuendelea hadi katikati ya jiji. Abiria wengi wamelazimika kushuka katika vituo vya mbali na kutembea kwa miguu kuingia mjini.
“Hatuelewi kinachoendelea, hatukupewa taarifa mapema. Tumetoka mbali, na sasa tunatembea kwa miguu hadi CBD,” alisema mmoja wa abiria aliyekuwa akitoka Thika, akiwa amesimama karibu na daraja la Pangani.
Katika eneo la Kangemi, magari ya kutoka mikoa ya magharibi na hata yale kutoka nchi jirani yalizuiwa kupita daraja kuu, na kusababisha abiria kushuka na kutafuta njia mbadala za kufika mjini. Wengi walionekana wakiwa wamebeba mizigo yao wakitembea kwa miguu, huku madereva wakielezea hasira zao kutokana na kukosa taarifa za mapema.
Katika barabara za Moi Avenue, Kenyatta Avenue na Tom Mboya, biashara nyingi zimefungwa, na maduka ya rejareja pamoja na vibanda vya wahudumu wadogo wa biashara vikiwa vimefungwa kabisa kwa hofu ya vurugu zinazoweza kutokea.
Katika mji wa Mombasa, hali kama hiyo pia imeshuhudiwa, hasa katika kituo cha reli cha Miritini, ambako abiria kadhaa walikwama usiku wa kuamkia leo baada ya polisi kufunga barabara ya Dongo Kundu. Taarifa kutoka kwa shirika la reli la Kenya zilieleza kuwa “SGR ya saa nane usiku iliondoka kama kawaida, lakini baadhi ya abiria walikosa kuwasili kwa wakati baada ya barabara kufungwa ghafla.”
Abiria kutoka kaunti ya Kwale walieleza kuchanganyikiwa huku wakilalamikia kukosa usafiri kutokana na vizuizi hivyo. “Tulifika Miritini tukiwa spidi ya dakika za mwisho, lakini polisi walikuwa wamefungwa barabara. Hakukuwa na maelekezo wala msaada,” alisema Asha Juma, msafiri kutoka Likoni.
Maandamano ya Saba Saba yamekuwa yakihusishwa na harakati za kudai mageuzi ya kikatiba na kijamii nchini Kenya tangu miaka ya 1990, na kila mwaka tarehe kama ya leo huwa na mvutano mkubwa kati ya raia na serikali. Mwaka huu, mashirika mbalimbali ya kijamii yameandaa maandamano kudai haki za kijamii, kupinga gharama ya juu ya maisha, na kutaka uwajibikaji wa viongozi wa umma.
Hadi sasa, serikali haijatoa taarifa rasmi kuhusu muda ambao vizuizi hivyo vitadumu, lakini taarifa za kiusalama zimeashiria kuwa hali hiyo inaweza kuendelea hadi jioni, kulingana na mwenendo wa maandamano.
Waangalizi wa haki za binadamu wametoa wito wa kuwepo kwa njia ya mawasiliano kati ya serikali na waandaaji wa maandamano ili kuepusha uvunjifu wa amani.
Pia wametoa tahadhari dhidi ya matumizi ya nguvu kupita kiasi na kukiukwa kwa haki za kiraia.
Kwa sasa, wakazi wa Nairobi na Mombasa wanaendelea kukabiliana na usumbufu mkubwa wa usafiri na shughuli za kila siku, huku taifa likisubiri kuona mwelekeo wa maandamano ya leo.


0 Comments:
Post a Comment