MBINU MPYA ZA KUINGIZA DAWA ZA KULEVYA KUPITIA MIFUKO YA MBOLEA YABAINIKA

 


Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola, imefanikiwa kukamata dawa haramu aina ya Mitragyna Speciosa zenye uzito wa kilo 11,031.42 katika kipindi cha Mei hadi Julai 2025. 



Dawa hizo zilibainika zikiingizwa nchini kwa ujanja mkubwa, ndani ya mifuko iliyokuwa na alama na maandishi ya mbolea.


Akizungumza jijini Dar es Salaam tarehe 9 Julai 2025, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, alisema dawa hiyo ni hatari sana kwa afya ya binadamu, kwani ina kemikali zinazoshambulia moja kwa moja mfumo wa fahamu.



“Mmea huu una kemikali hatari zinazoweza kuathiri mfumo wa fahamu na kusababisha uraibu na vifo vya ghafla,” alisema Lyimo.

Alifafanua kuwa Mitragyna Speciosa, inayojulikana pia kama Kratom, huonekana kwa mtumiaji kama kichangamshi kwa awali, lakini baadaye hupelekea kupooza kwa fahamu, na matumizi ya muda mrefu huleta utegemezi mkubwa na hatari ya kupoteza maisha.

Kamishna Lyimo alibainisha kuwa mamlaka yake itaendelea kuimarisha udhibiti katika maeneo yote ya mipaka ya nchi, ikiwa ni pamoja na bandari na viwanja vya ndege, ili kukabiliana na mbinu mpya zinazotumiwa kuingiza dawa hizo.

“DCEA itaendelea kuimarisha udhibiti katika maeneo yote ya mipaka na kubaini mbinu mpya zinazotumiwa kuingiza dawa hizo nchini,” aliongeza.

Katika kipindi hicho hicho, DCEA pia ilikamata dawa nyingine haramu zikiwemo bangi kilo 24,873.56, mirungi kilo 1,274.47, skanka kilo 13.42, heroin kilo 2.21, methamphetamine gramu 1.42, ketamine kilo 1.92 pamoja na vidonge 1,000 vya Rohypnol na lita 6 za acid hydrochloric.

Aidha, mashamba makubwa ya bangi yaliteketezwa katika mikoa ya Ruvuma, Mbeya, Mara, Kagera, Dodoma, Tabora, Morogoro na Arusha, na watu 64 walikamatwa kwa tuhuma mbalimbali zinazohusiana na biashara na matumizi ya dawa hizo.

Kamishna Lyimo alitoa wito kwa wananchi kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa za siri kuhusu watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya ili kulinda jamii na kizazi kijacho dhidi ya janga hili.

“Tunaendelea kuomba wananchi kuelekeza mashaka yao kuhusu watu wanaojihusisha na biashara hii haramu, ili tuweze kuokoa jamii,” alihimiza.

Hili ni onyo kwa wale wote wanaotafuta njia za ujanja kuharibu maisha ya wengine, huku mamlaka zikiwa makini kubaini na kuvunja kila mnyororo wa usambazaji wa dawa haramu nchini.

0 Comments:

Post a Comment