Mashabiki wa PSG Wazua Vurugu Baada ya Ushindi wa 5-0 Dhidi ya Inter Milan, Watu Wawili Wapoteza Maisha

 


Zaidi ya watu 500 wamekamatwa nchini Ufaransa kufuatia vurugu zilizozuka baada ya klabu ya Paris Saint-Germain (PSG) kuibuka na ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya Inter Milan katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA Champions League) iliyochezwa mjini Munich, Ujerumani.



Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ufaransa, watu 491 walikamatwa jijini Paris pekee baada ya mashabiki wa PSG kuvamia mitaa na kuanzisha fujo katika maeneo mbalimbali, yakiwemo Champs-Elysee na karibu na uwanja wa Parc des Princes ambako zaidi ya mashabiki 48,000 walikuwa wamekusanyika kutazama mchezo huo kupitia skrini kubwa.



“Tumesikitishwa na matukio ya vurugu yaliyotokea baada ya ushindi mkubwa wa PSG. Tunalaani vikali vitendo vya uharibifu wa mali na vurugu dhidi ya askari wetu,” ilisema taarifa rasmi ya Wizara hiyo.

Matukio hayo ya kushangaza yamesababisha vifo vya watu wawili. Mmoja alifariki baada ya kugongwa na gari katika eneo la kusini mwa Paris, na kijana mwingine mwenye umri wa miaka 17 aliuawa kwa kuchomwa kisu wakati wa sherehe za mashabiki katika mji wa Dax, Kusini Magharibi mwa Ufaransa.

Polisi wa Jiji la Paris kupitia msemaji wao wamesema:

“Vurugu kubwa ziliripotiwa hasa katika maeneo ya Champs-Elysee, ambapo tulilazimika kutumia vikosi vya ziada kuzuia uharibifu zaidi wa mali na kulinda usalama wa raia.”

Kufikia leo Jumapili, idadi ya waliokamatwa imeongezeka hadi 559 kote nchini, huku vyombo vya usalama vikiendelea kuimarisha doria.

Licha ya vurugu hizo, PSG imepanga kuandaa gwaride maalum la ushindi leo hii katika barabara maarufu ya Champs-Elysee, ambapo maelfu ya mashabiki wanatarajiwa kujitokeza kushuhudia mashujaa wao wa soka.

Ikulu ya Ufaransa imethibitisha kuwa Rais Emmanuel Macron atakutana na wachezaji wa PSG kuwapongeza kwa mafanikio hayo makubwa.

“Rais anawapongeza PSG kwa ushindi wa kihistoria na atakutana nao rasmi leo hii kuwapa heshima wanayostahili,” imesema taarifa kutoka ofisi ya rais.

Taarifa zinaeleza kuwa zaidi ya watu milioni 11.5 waliufuatilia mchezo huo kupitia televisheni ndani ya Ufaransa, ikiwa ni rekodi ya juu ya watazamaji kwa fainali ya Champions League kwa mwaka huu.


Mashabiki wa PSG waliifurahia mechi hiyo kwa shangwe, nyimbo, na mapokezi ya kishujaa, lakini vurugu zilizofuatia zimetia doa kwenye ushindi huo wa kihistoria. Polisi na viongozi wa serikali wametoa wito kwa mashabiki kusherehekea kwa amani na kwa kuzingatia sheria.

0 Comments:

Post a Comment