Mvutano Mkali wa Kisheria Waibuka Kesi ya Tundu Lissu Kisutu – “No Reform, No Election” Yaleta shida mahakamani

 



Kesi ya uhaini na kuchapisha taarifa za uongo inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Antipas Lissu, imeendelea kusikika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, huku pande zote mbili – Jamhuri na utetezi – zikijikuta katika mvutano mkali kuhusu hatua ya upelelezi na ulinzi wa mashahidi.



Lissu alifikishwa mahakamani saa 2:28 asubuhi chini ya ulinzi mkali wa polisi waliokuwa na silaha nzito na mbwa wa kazi, akiwa ameambatana na jopo la mawakili wake. Alipoingia mahakamani, alionyesha alama ya vidole viwili – ishara ya kaulimbiu ya CHADEMA – na kuwasalimia wafuasi wake waliokuwepo kwa kuwapa mikono. 


Wafuasi hao walipaza kauli ya “No reform, no election” kabla ya kesi kuanza, hali iliyomwinua Wakili wa Serikali, Nasoro Katuga.

“Kwa sababu upelelezi wa shauri hili bado unaendelea baada ya jalada kupelekwa ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kusomwa na kuona bado kuna mapungufu machache ya kumalizia,” alisema Wakili Katuga.

Utetezi Wataka Upelelezi Wasilishwe

Wakili wa Lissu, Jeremiah Mtobesya, alipinga hoja hiyo akisema ni njia ya kuchelewesha kesi isiyo ya lazima.

“Tunaomba mahakama hii ione hivyo kwamba ni ucheleweshaji usioweza kuvumilika. Nimekumbushwa na wenzangu hapa kuwa kwa kuwa mtuhumiwa ana kesi mbili, mbona ile nyingine upelelezi umekamilika?” alihoji Mtobesya.

Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga, aliitaka Jamhuri kufafanua hatua halisi ya kesi hiyo na kuahirisha hadi Juni 1, 2025, akisisitiza kuwa upelelezi ukamilishwe mapema.

Katika kesi ya uchapishaji taarifa za uongo, upande wa Jamhuri uliwasilisha ombi jipya la kuficha mashahidi 15, wakieleza kuwa wamefungua maombi rasmi mbele ya Hakimu mwingine kwa mujibu wa Kifungu cha 188(1) na 392(A) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

“Mheshimiwa, tunaomba ahirisho la kesi hii kwa sababu tumewasilisha maombi ya kulindwa kwa mashahidi... uamuzi wa Mahakama kuhusu maombi hayo unaweza kuwa na athari kubwa kwenye mwenendo wa kesi nzima,” alieleza Katuga.

Upande wa Utetezi Wapinga Vikali

Jopo la mawakili 30 wanaomtetea Lissu walipinga vikali ombi hilo, wakidai ni njama ya kuendesha kesi kwa usiri usio wa kisheria.

“Hatuwezi kuahirisha kesi kusubiri tukio ambalo halijatokea... huu si msingi wa sheria. Kama hawapo tayari kuendelea, Mahakama ifute mashtaka na imuachie mshtakiwa,” alisema Wakili Mtobesya.

Wakili Peter Kibatala naye aliongeza kuwa:

“Tunauliza, huu ndiyo msimamo wa DPP? Kama sisi tungedharau amri ya Mahakama, ingekuaje? Lazima amri za Mahakama ziheshimiwe.”

Wakili Dk. Rugemeleza Nshalla naye alionya kuwa kuchelewesha mwenendo wa kesi huondoa imani kwa wananchi.

“Kuzunguka zunguka na kuchelewesha mwenendo wa kesi kunawafanya wananchi kuona kama kuna mambo yanayofichwa,” alisema Dk. Nshalla.

Kwa upande wake, Katuga alijibu kwa kusema:

“Sijui wanang’ang’ania taarifa za mashahidi za nini, huyu ni mtoa taarifa. Kama DPP ataona shahidi anatakiwa kulindwa, analeta maombi, ndivyo alivyofanya... kesi haiwezi kufutwa kwa sababu mlalamikaji yupo na ni Jamhuri.”

Mahakama Yatoa Uamuzi

Hakimu Geofrey Mhini, baada ya kuandika uamuzi wake kwa zaidi ya saa moja, alikubaliana na hoja za upande wa Jamhuri na kuahirisha kesi hadi Juni 16, 2025.

“Kwa busara ya Mahakama, ninaona ni bora niahirishe kesi hii ili kutoa nafasi ya kusikilizwa kwa maombi ya upande wa Jamhuri,” alisema Mhini.

Kesi na Mashtaka Yanayomkabili Lissu

Katika kesi hiyo, Lissu anatuhumiwa kuchapisha taarifa za uongo kupitia YouTube mnamo Aprili 3, 2025, ikiwa ni pamoja na madai kwamba:

  • “Uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka jana, wagombea wa Chadema walienguliwa kwa maelekezo ya Rais.”

  • “Polisi wanatumika kuiba kura wakiwa na vibegi.”

  • “Majaji ni Ma-CCM hawawezi kutenda haki wanapenda wapate teuzi kuchaguliwa kuwa majaji wa Mahakama ya Rufaa.”

Lissu aliachiwa kwa dhamana kwa sharti la kuwa na mdhamini mmoja aliyesaini bondi ya Shilingi milioni tano na kuwasilisha kitambulisho cha taifa (NIDA).


Hata hivyo anaendelea kuwa mahabusu gerezaji kutokana na kesi ya uhaini ambayo haina dhamana.

Makala hii itaendelea kuangazia kesi hii ya kihistoria inayobeba uzito mkubwa wa kisiasa na kisheria nchini Tanzania.

0 Comments:

Post a Comment