Wanafunzi Wanaodaiwa Kumshambulia Mwenzao kwa Wivu wa Mwijaku Waburuzwa Mahakamani

  


Wanafunzi watatu wa kike kutoka vyuo vikuu mbalimbali jijini Dar es Salaam wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka nane, yakiwemo kula njama, kuchapisha taarifa za uongo, kushambulia kwa kutumia chuma, na kutishia kuua kwa kisu.




Washtakiwa hao ni Mary Matogoro (22), mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mkazi wa Sinza, Ryner Mkwawili (22), mwanafunzi wa Chuo Kikuu Ardhi mkazi wa Makongo, na Asha Juma (22), mwanafunzi wa Chuo cha Uhasibu Dar es Salaam mkazi wa Kigamboni.

Wakisomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Gwantwa Mwankuga, wakili wa serikali Tumaini Mafuru alidai kuwa mnamo Machi 16, 2025, katika eneo la Sinza, Wilaya ya Ubungo, washtakiwa hao walikula njama ya kuchapisha taarifa za uongo dhidi ya mwenzao, Magnificat Kimario.

Katika shtaka la pili, ilidaiwa kuwa Mary Matogoro na Asha Juma walichapisha taarifa za uongo katika mfumo wa kompyuta kupitia mtandao wa WhatsApp, wakimkashifu Kimario kwa maneno ya matusi yaliyoelekezwa moja kwa moja kwake. 


"Toa sauti umefuck na mpenzi wa Mwijaku lini, umefuck nae wapi?" ilisomeka sehemu ya ujumbe uliodaiwa kusambazwa na washtakiwa hao.

Ilidaiwa pia kuwa siku hiyo hiyo, Machi 16, 2025, Mary Matogoro alimshambulia Kimario kwa kutumia chuma kichwani, hali iliyosababisha majeraha makubwa katika sehemu ya kichwa.

Katika shtaka jingine, washtakiwa wanadaiwa kumsababishia Kimario madhara kwa kumvuta nywele kwa nguvu. Mary Matogoro pia anadaiwa kuharibu laini ya simu iliyosajiliwa kwa jina la Kimario bila sababu ya msingi.

Shtaka la saba linadai kuwa Mary Matogoro aliharibu simu ya Kimario yenye thamani ya shilingi 700,000. Katika shtaka la nane, washtakiwa wote wanadaiwa kumtishia Kimario kwa kisu wakimtishia kumuua.

Washtakiwa wote walikana mashtaka yote yaliyosomwa dhidi yao.

Mahakama imewawekea masharti ya dhamana kwa kuwa na wadhamini wawili kila mmoja, wenye vitambulisho vya Taifa (NIDA) na barua za utambulisho kutoka serikali za mitaa. Hadi kufikia mwisho wa muda wa kusikilizwa kwa kesi hiyo siku ya Ijumaa, ni Mary Matogoro pekee aliyekuwa hajatimiza masharti ya dhamana, huku wenzake wawili wakifanikiwa.

Wakili wa Serikali, Tumaini Mafuru, alisema kuwa “Upelelezi wa kesi hii bado unaendelea.”

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 13, 2025, itakapotajwa tena mahakamani.

0 Comments:

Post a Comment