Doroth Aomba Ridhaa ya ACT Wazalendo Kugombea Urais

 

Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Doroth Semu, ameomba ridhaa ya chama chake ili kuwania nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.



Akizungumza leo jijini Dar es Salaam mbele ya waandishi wa habari na wanachama wa chama hicho, Semu alisema amefikia uamuzi huo baada ya kutathmini hali ya sasa ya taifa na kuona haja ya kuwepo kwa mabadiliko ya uongozi.

"Tuna kazi moja kubwa — kuiondoa CCM madarakani na kuijenga Tanzania mpya kwa misingi ya haki, usawa, uongozi wa uwazi, na uchumi wa watu. Ndiyo dhamira yangu kuu," alisema Semu.



Katika hotuba yake, alieleza kuwa ajenda yake kuu ni kuijenga Tanzania mpya yenye uchumi jumuishi na haki kwa wote, huku akitaja maeneo manne ya kipaumbele:

1. Kujenga Uchumi Jumuishi, Imara na Unaostawi
"Tutawainua Watanzania hasa vijana na wanawake kwa kuwawekea mazingira ya kupata ajira zenye kipato cha heshima," alisema Semu.

Ameeleza kuwa atahakikisha:

  • Uwekezaji unafanyika kwenye sekta zenye ajira nyingi kama kilimo, ufugaji, uvuvi na biashara ndogondogo.

  • Mifumo ya biashara na ujasiriamali inaimarishwa kwa urahisi wa upatikanaji wa mitaji.

  • Mifumo ya kodi na urasimishaji inaboreshwa ili kuhamasisha ukuaji wa uchumi.

  • Huduma bora za jamii zinatolewa kwa kila Mtanzania bila ubaguzi.

  • Mfumo wa Hifadhi ya Jamii unaboreshwa, ukiwemo mfuko wa afya na pensheni ya taifa.



2. Usimamizi Madhubuti wa Rasilimali za Taifa
"Tutahakikisha rasilimali za taifa zinawanufaisha wananchi wa sasa na vizazi vijavyo," alisema.

Aliahidi kuweka sheria ya ushirikishwaji wa wananchi katika miradi ya uchimbaji wa rasilimali na kusimamia kwa ukamilifu matumizi yake.

3. Mapambano Dhidi ya Rushwa, Uzembe na Ubadhirifu
"Wale wote waliotajwa katika taarifa za CAG watawajibishwa bila kuficha," alisema Semu.

Pia alieleza nia ya kupunguza matumizi ya anasa kwa viongozi na kuelekeza rasilimali hizo kwenye huduma kwa wananchi na miradi ya maendeleo.

4. Kuimarisha Demokrasia na Haki za Raia
"Tutapigania uchaguzi huru na wa haki, na kulinda thamani ya kura ya kila Mtanzania," alisisitiza.

Semu alisema atahakikisha wananchi wanarudishiwa imani yao kwa taasisi za uchaguzi na mfumo wa vyama vingi.

Akihitimisha hotuba yake, Semu alitoa wito kwa Watanzania wote kushiriki katika mchakato wa mabadiliko ya kweli.

0 Comments:

Post a Comment