Wanandoa wawili, Geofrey Anael Mota (60) na Blandina Felix Ngowi (53), wakazi wa Mtaa wa Msufini, Kata ya Msaranga, Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wameuawa kikatili na watu wasiojulikana usiku wa Mei 29, 2025, na tukio hilo limezua taharuki miongoni mwa wakazi wa eneo hilo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, marehemu Geofrey alikutwa amekatwa na kitu chenye ncha kali shingoni huku mwili wa mke wake, Blandina, ukikutwa bila majeraha yoyote ya wazi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mei 30, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Simon Maigwa, amesema:
“Tukio hilo limetokea ndani ya nyumba ya kupanga waliokuwa wakiishi wanandoa hao pamoja na kijana wao wa kiume (jina lake tunalihifadhi) ambaye ametoweka baada ya mauaji hayo kutokea.”
Kamanda Maigwa aliongeza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na msako mkali kuwasaka wote waliohusika katika tukio hilo la mauaji ya kikatili.
“Tunaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha tukio hili pamoja na kuwakamata wote waliohusika na mauaji haya,” amesema Kamanda Maigwa.
Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) kwa ajili ya uchunguzi wa kitabibu na taratibu nyingine za mazishi.
Tukio hilo limezua maswali mengi kwa wakazi wa eneo hilo, hususan kuhusu sababu ya mauaji hayo na kutoweka kwa kijana wa familia hiyo, ambaye hadi sasa hajapatikana.
Jeshi la Polisi limewahakikishia wananchi kuwa litaendelea kufuatilia kwa karibu suala hilo na kutoa taarifa zaidi mara uchunguzi utakapokamilika.

0 Comments:
Post a Comment