Serikali ya Uingereza imepanga kuanzisha rasmi matumizi ya dawa za kuzuia hamu ya ngono kwa watu waliohukumiwa kwa makosa ya kingono, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kupunguza uwezekano wa wahalifu hao kurudia makosa na kupunguza msongamano kwenye magereza.
Waziri wa Sheria wa Uingereza, Shabana Mahmood, alitoa taarifa hiyo bungeni Alhamisi, kufuatia mapitio huru ya mfumo wa utoaji wa hukumu kwa wahalifu wa kingono.
“Kile kinachojulikana kama kuhasiwa kwa kemikali kitatumika katika magereza 20 katika mikoa miwili,” alisema Mahmood, na kuongeza kuwa, “ninafikiria kuifanya kuwa kitendo cha lazima.”
Kuhasiwa kwa kutumia kemikali kunahusisha matumizi ya dawa maalum zinazopunguza hamu ya ngono, kwa kushirikiana na tiba ya akili, na huelekezwa kwa wahalifu wenye matatizo ya kiakili au fikra potofu kuhusu ngono.
“Kwa kweli, ni muhimu kwamba mbinu hii ichukuliwe sambamba na mbinu za kisaikolojia ambazo zinalenga sababu nyingine za kuudhi, kama vile kuzuwia na udhibiti wa ngono,” alisema Mahmood.
Waziri huyo alibainisha kuwa si kila mkosaji wa kingono atawekewa matibabu hayo, kwani baadhi kama wabakaji ambao motisha yao ni mamlaka au udhibiti, si lazima wawe na matatizo ya tamaa ya ngono.
“Ni muhimu kwa mbinu hii kutekelezwa pamoja na hatua za kisaikolojia ambazo zinalenga kutibu sababu zingine za kosa la kingono, kama vile mtu kutaka kumdhibiti mwingine au kuwa na nguvu zaidi yake,” alisisitiza.
Utafiti uliotolewa katika mapitio hayo ulionyesha kuwa kuhasi kwa kemikali kunaweza kupunguza uwezekano wa kurudia kosa la kingono kwa asilimia hadi 60.
Hatua kama hii ya matibabu pia hutekelezwa kwa hiari nchini Ujerumani na Denmark, huku nchini Poland ikifanyika kwa lazima.
Uamuzi huu wa Uingereza unalenga kutafuta njia za ufanisi zaidi za kushughulikia uhalifu wa kingono na kulinda usalama wa jamii kwa kutumia mbinu za kisasa na za kitabibu.

0 Comments:
Post a Comment