ALMASI YENYE THAMANI YA ZAIDI YA BILIONI 1.7 YAKAMATWA IKITOROSHWA

 

Serikali imekamata almasi yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 1.7 ikisafirishwa kinyume cha sheria katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kudhibiti utoroshaji wa madini nchini.



Akizungumza na waandishi wa habari Mei 24, 2025 katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, alithibitisha kuwa madini hayo yalinaswa Mei 18, yakisafirishwa na raia wa kigeni wakiwa na mabegi manne yaliyokuwa yamefichwa madini hayo.

"Madini haya yamekamatwa yakisafirishwa kinyume na utaratibu na raia wa kigeni, yakiwa kwenye mabegi manne katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza," alisema Mavunde.

Ameeleza kuwa Serikali imesikitishwa sana na kitendo hicho na kwamba haitavumilia kabisa tabia ya baadhi ya watu kujaribu kuiba rasilimali za nchi.

"Serikali inalaani vikali vitendo vya namna hii vya utoroshwaji wa madini. Hatutavumilia kuona mali ya nchi ikiporwa kwa maslahi ya watu wachache," alisisitiza.



Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde alieleza mafanikio ya Serikali katika ukusanyaji wa mapato kupitia sekta ya madini, akifichua ongezeko kubwa la mapato ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

“Kwa mwaka wa fedha 2015/2016 tulikusanya bilioni 162 kutokana na biashara ya madini. Lakini kutokana na udhibiti mkubwa dhidi ya utoroshaji wa madini, hadi kufikia Mei mwaka wa fedha 2024/2025 tumeshakusanya shilingi bilioni 925, na lengo letu ni kufikisha trilioni moja,” alisema.

Tukio hilo limeendelea kuonyesha umuhimu wa kuimarisha mifumo ya ulinzi wa rasilimali za taifa na kuwachukulia hatua kali wale wote wanaojihusisha na vitendo vya kihalifu katika sekta ya madini.

0 Comments:

Post a Comment