Chama cha ACT-Wazalendo kimetangaza kuwa kiko tayari kushiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa dhamira ya dhati ya kuendeleza harakati za mabadiliko ya kweli, kulinda haki za wananchi, na kuendeleza mapambano ya ukombozi wa Taifa.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mei 24, 2025, katika viwanja vya shule ya Msingi Town, Manispaa ya Shinyanga, Mwenyekiti wa chama hicho Taifa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, amesema kuwa msingi wa kuasisi Taifa hili ulikuwa ni kuwapatia wananchi uhuru, sauti, na heshima ya kufanya maamuzi, lakini dhamira hiyo imepotea kwa sababu ya mfumo wa sasa wa utawala.
"Lile ambalo tulilipambania sasa halipo tena, na wenzetu ndio ambao wamelipoteza," amesema Othman kwa msisitizo, akisisitiza kuwa kunyimwa kwa wananchi haki ya kuchagua ni sawa na kuwakosesha utu wao.
Ameeleza kuwa Shinyanga na maeneo ya jirani yana utajiri mkubwa wa rasilimali kama dhahabu na almasi, lakini wananchi wake wanaendelea kuwa maskini kutokana na matumizi mabaya ya rasilimali hizo. "Shinyanga kama ingekuwa nchi inayojitegemea, ingeweza hata kuikopesha Tanzania nzima," amesema.
Katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, alimpongeza Othman kwa kusimamia misingi ya haki bila kuyumba na aliwapokea wanachama wapya 26 kutoka vyama vingine vya upinzani.
Ziara hiyo ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya ACT-Wazalendo iitwayo Operesheni Linda Demokrasia, yenye lengo la kufufua matumaini ya wananchi na kuhakikisha sauti zao zinasikika kupitia uchaguzi wa haki.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na viongozi wa kitaifa na wa Kanda ya Ziwa, wakiwemo wajumbe wa Kamati Kuu, Halmashauri Kuu, na Mwenyekiti wa chama mkoa wa Shinyanga, Hassan Ibrahim.



0 Comments:
Post a Comment