“TUSIGWAJIMANISE CHAMA CHETU” – SAMIA AMSHUKIA GWAJIMA, CCM YAZINDUA ILANI YENYE SERA 9 ZA MAGEUZI



Tukitoa mwanya na kupitisha wanaotafuta tu, na mie niwemo, ndiyo tunapata wale waokwenda huko, Chama kinakuwa Gwajimanised. Kwa namna yoyote, tusigwajimanise Chama chetu, magwajima tuyaache nje. Hakuna kuoneana aibu wala haya.”



Kauli hiyo kali imetolewa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, akielekeza lawama kwa viongozi wa chama wanaoshindwa kufanya mchujo wa haki na badala yake kuendekeza ushawishi wa muda mfupi unaozaa wagombea wasiokuwa na uhusiano wa kweli na chama.

Amesema hayo Mei 30, 2025 jijini Dodoma wakati wa kufunga Mkutano Maalum wa CCM uliofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre (JKCC), ambapo chama hicho pia kilizindua Ilani yake ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Samia amesisitiza kuwa vikao vya uteuzi havipaswi kufanyika kwa upendeleo wala mashinikizo kutoka kwa makundi ya maslahi binafsi, bali kwa kuzingatia sifa, uwezo na maadili ya wagombea.

Vikao vinavyokwenda kuchuja watu, vinavyokwenda kuchuja wagombea, wakatende haki. Anayefaa aambiwe anafaa, asiyefaa tuseme huyu ana kasoro moja mbili tatu, hatufai huko mbele tunapokwenda.”

Aidha, ameonya kuwa mtu asiye na uhusiano wa kweli na chama ni hatari kwa uhai wa CCM:

Mcheza ngoma si yake lazima ataharibu, ukicheza ngoma si yako utaharibu na utajulikana tu.”

ILANI YA CCM 2025: SERA TISA ZA KUIJENGA TANZANIA MPYA

Wakati huo huo, Chama Cha Mapinduzi kilizindua Ilani yake ya Uchaguzi kwa mwaka 2025 yenye vipaumbele tisa vinavyolenga kuleta mageuzi ya kiuchumi, kijamii na kisiasa, ikiwemo dhamira ya kuhuisha mchakato wa katiba mpya.

Akiwasilisha Ilani hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Mipango na Uwekezaji, Kitila Mkumbo, alisema:

Ilani hii imeandaliwa kwa makini kwa kuzingatia changamoto za sasa, fursa zilizopo, na matarajio ya Watanzania kwa miaka ijayo.”

Vipaumbele 9 vya Ilani ya CCM 2025 ni pamoja na:

  1. Kuchochea Mapinduzi ya Uchumi wa Kisasa

  2. Kuongeza Fursa za Ajira kwa Vijana na Kupunguza Umaskini

  3. Kuboresha Maisha ya Watu na Ustawi wa Jamii

  4. Kuimarisha Miundombinu ya Usafiri na Usafirishaji

  5. Kukuza na Kuimarisha Matumizi ya Sayansi na Teknolojia

  6. Kudumisha Demokrasia, Utawala Bora na Uwajibikaji

  7. Kuendelea Kudumisha Amani, Utulivu na Usalama

  8. Kudumisha Utamaduni wa Kitaifa na Kukuza Sanaa na Michezo

  9. Kuongeza Kasi ya Maendeleo Vijijini

Katika kipengele cha “Kudumisha Demokrasia na Utawala Bora,” Ilani hiyo inaeleza:

CCM inaamini kuwa misingi imara ya utawala bora, demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria ni muhimu katika kuhakikisha Taifa linaendelea kuwa na amani na utulivu.”

Pia, Ilani hiyo imeainisha mafanikio kama kupitishwa kwa Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi ya 2024, ambayo imeondoa kipengele cha wagombea kupita bila kupingwa na kuweka mfumo wa usaili wa wajumbe wa tume hiyo, ikiwa ni hatua muhimu katika kuimarisha demokrasia.

Kadhalika, imeahidi kuendeleza uhuru wa vyombo vya habari, ushiriki wa wananchi katika masuala ya umma na kuimarisha nafasi ya asasi za kiraia kwa ajili ya kuongeza uwajibikaji wa viongozi.

Kwa ujumla, kauli ya Samia imeibua mjadala mpana ndani na nje ya chama, hasa kutokana na rejea yake kwa “magwajima” kama mfano wa viongozi au wagombea wanaotia doa CCM. 



0 Comments:

Post a Comment