KABILA AIBUKA GOMA, AKUTANA NA VIONGOZI WA DINI – AAHIDI KUSAIDIA KUREJESHA AMANI

 


Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Joseph Kabila Kabange, alikutana siku ya Alhamisi na viongozi wa kidini katika mji wa Goma – miongoni mwa ngome zinazodhibitiwa na waasi wa M23 – akielezea dhamira yake ya kusaidia kurejesha amani katika eneo hilo lenye misukosuko.



Katika kile kinachoonekana kama kurejea kwa tahadhari kwenye jukwaa la kisiasa, Kabila alisema ziara yake si ya kisiasa bali ya utu na mshikamano wa kitaifa.



“Nimerudi kama raia mwenye uchungu na hatima ya taifa letu. Goma ni sehemu ya moyo wa Kongo – na amani yake ni amani ya nchi nzima,” alisema Kabila wakati wa kikao kilichofanyika katika moja ya makaazi yake mjini humo.

Viongozi wa dini waliohudhuria kikao hicho walimkaribisha kwa tahadhari lakini walitambua uzito wa hatua hiyo. Askofu Mkuu Joel Amurani wa Jukwaa la Madhehebu ya Dini alisema:

“Tumemweleza kwamba bado ana nafasi ya kuwa mpatanishi. Kwa miaka 18 alilitumikia taifa, na bado anaweza kulisaidia kurejea katika umoja na mshikamano.”

Wakati Kabila akionyesha ishara ya upatanishi, Serikali ya Rais Félix Tshisekedi kupitia Waziri wa Sheria Constant Mutamba imeendelea kusisitiza kwamba hakuna mtu aliye juu ya sheria. 


Kabila anatuhumiwa kuhusika kwa njia isiyo ya moja kwa moja na waasi wa M23 wanaodaiwa kupata msaada kutoka Rwanda.

“Hatufungii macho uhalifu wa kivita, uasi na mateso ya raia. Uchunguzi unafanyika, na iwapo atahusishwa moja kwa moja, sheria itafuata mkondo wake,” alieleza Mutamba kwa waandishi wa habari mjini Kinshasa.

Baadhi ya wachambuzi wa siasa wanasema kurejea kwa Kabila Goma, mji uliogubikwa na mgogoro wa kibinadamu na hali duni ya kiusalama, ni mkakati wa kujenga taswira mpya kisiasa, hasa baada ya kuondolewa kinga ya “seneta wa maisha” wiki iliyopita.

Mashariki mwa Kongo kwa sasa inakabiliwa na hali mbaya ya kibinadamu huku mamilioni ya raia wakiwa wakimbizi wa ndani. Mapigano kati ya waasi wa M23 na jeshi la serikali yameendelea licha ya juhudi za kidiplomasia na kijeshi.

“Tunahitaji kurejea kwenye mazungumzo. Tusijifiche nyuma ya siasa au silaha. Huu ni wakati wa kuponya taifa letu,” alisisitiza Kabila akihitimisha mkutano wake na viongozi wa dini.

Kwa sasa, macho ya wengi yameelekezwa mashariki mwa Kongo kuona iwapo kurejea kwa Kabila kutachochea mabadiliko ya kweli au kuzua sura mpya ya mvutano wa kisiasa.


0 Comments:

Post a Comment