Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa majibu rasmi kwa mwanachama wake, Lembrus Mchome, kikieleza kuwa kikao cha Baraza Kuu la Taifa kilichofanyika hivi karibuni kilikuwa halali na kilitimiza vigezo vyote vya kikatiba, ikiwemo akidi ya wajumbe.
Kupitia barua yenye kumbukumbu namba C/HQ/ADM/SG/02 ya Februari 20, 2025, iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika, CHADEMA imekanusha hoja zote nane zilizowasilishwa na Mchome kuhusu uhalali wa kikao hicho, kikisema kuwa, “Sababu zote nilizozitaja hapo juu, malalamiko na maombi yako yote hayana ukweli wala msingi wowote.”
Mchome alikuwa amedai kuwa idadi ya wajumbe halali wa Baraza Kuu waliohudhuria kikao hicho ni 234, sawa na asilimia 56.8 ya wajumbe wote, na kwamba kiwango hicho hakikufikia akidi inayohitajika kwa mujibu wa Katiba ya chama.
Unaweza kusoma zaidi
https://habaritanzaniagracemacha.blogspot.com/2025/05/msajili-atengua-uteuzi-wa-viongozi-nane.html
Hata hivyo, katika majibu yake, Mnyika alieleza kuwa, “Kikao unachokilalamikia kilikuwa ni kikao cha kawaida cha Baraza Kuu kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya kawaida, kama vile kuthibitisha jina la Katibu Mkuu, manaibu wake na wajumbe wa Kamati Kuu walioteuliwa na Mwenyekiti wa Chama.”
Aliongeza kuwa kwa mujibu wa ibara ya 6.2.2(a) ya Katiba ya CHADEMA, kikao cha kawaida cha Baraza Kuu kinahitaji akidi ya angalau asilimia 50 ya wajumbe wote, na hivyo asilimia 56.8 iliyohudhuria inakidhi matakwa ya Katiba.
Kuhusu madai kuwa baadhi ya waliokuwepo kwenye kikao hicho hawakuwa wajumbe halali, Mnyika alieleza: “Lilian Masiaga na Injinia Dk. Nyamatari Tengecha si wajumbe wa Baraza Kuu na hawapo kwenye orodha ya mahudhurio. Kwa hiyo, kuwepo au kutokuwepo kwao hakuwezi kuathiri akidi wala kubatilisha maamuzi yaliyofanyika.”
Pia alibainisha kuwa Mchome mwenyewe hakuhudhuria kikao hicho, akisema: “Kwa hiyo, inaelekea malalamiko yako yametokana na maneno ya kuambiwa ama ya kuhisi, lakini yasiyokuwa na ukweli au msingi wowote.”
Mnyika alihitimisha kwa kutoa wito kwa wanachama kuwa makini na upotoshaji: “Ingependeza sana kama mwanachama na kiongozi wa chama kama ungetafuta ukweli wa jambo hili kwenye ofisi yangu kwanza kabla ya kuandika na kusambaza uzushi huu mitandaoni na kwenye vyombo vya habari na hivyo kuleta taharuki ya bure kwa wanachama na wananchi.”

0 Comments:
Post a Comment