Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimejibu kwa nguvu mbili tofauti tuhuma dhidi ya uhalali wa viongozi wake—moja ikielekezwa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, na nyingine kwa mwanachama wake Lembrus Mchome—kikisisitiza kuwa viongozi wake waliteuliwa kwa kufuata katiba na taratibu zote halali za chama.
Kupitia tamko rasmi lililotolewa baada ya Msajili kutangaza kutowatambua viongozi kadhaa wa CHADEMA walioteuliwa baada ya uchaguzi wa ndani wa chama uliofanyika Januari 22, 2025, chama hicho kimesema hatua hiyo ni ya kisiasa na inalenga kudhoofisha harakati za chama hicho cha upinzani.
Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, John Heche, ambaye kwa sasa anaendelea na ziara ya kuhamasisha ajenda ya chama ya “Bila Mabadiliko Hakuna Uchaguzi”, alisema:
“Kumekuwa na mbinu chafu zinazoendelea kuratibiwa ili kuivuruga CHADEMA ambayo inaendelea kuandamwa na mfululizo wa matukio.”
Akizungumzia hatua ya Msajili kutowatambua viongozi wa sekretarieti ya chama akiwemo Katibu Mkuu John Mnyika, Heche alisema:
“Msajili huitaji kumtambua Katibu Mkuu wa chama chetu. Sisi CHADEMA tunamtambua Katibu Mkuu wa chama chetu.”
Kwa upande wake, Katibu Mkuu John Mnyika alisema kuwa hatua hiyo haitadhoofisha msimamo wa chama, bali itaamsha nguvu mpya za kisiasa na kisheria.
“Nataka kuwaambia waliotumwa: Hii mbinu nayo itashindwa. Safu yetu ya mawakili imekwisha jipanga kwa mapambano mahakamani,” alisema Mnyika.
Katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu Bara, Amani Golugwa, alikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere Jumatatu usiku, kwa madai ya kusafiri mara kwa mara nje ya nchi bila kufuata utaratibu. Aliachiliwa usiku huo huo, pamoja na viongozi wengine wa CHADEMA waliokwenda kumwekea dhamana na waliokamatwa kwa muda mfupi.
Golugwa alikuwa akielekea Brussels, Ubelgiji kuhudhuria mkutano wa Umoja wa Watetezi wa Demokrasia Duniani (IDU).
Wakati huo huo, CHADEMA pia kimetoa majibu rasmi kwa mwanachama wake Lembrus Mchome aliyehoji uhalali wa kikao cha Baraza Kuu la Taifa kilichowathibitisha baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho.
Kupitia barua yenye kumbukumbu namba C/HQ/ADM/SG/02 ya Februari 20, 2025, iliyosainiwa na Katibu Mkuu John Mnyika, chama kilimjibu Mchome kuwa kikao hicho kilikuwa halali na kilitimiza akidi inayohitajika kwa mujibu wa katiba.
“Sababu zote nilizozitaja hapo juu, malalamiko na maombi yako yote hayana ukweli wala msingi wowote,” alisema Mnyika katika barua hiyo.
Mchome alidai kuwa akidi ya kikao hicho haikufikiwa, lakini Mnyika alifafanua kuwa:
“Kikao unachokilalamikia kilikuwa ni kikao cha kawaida cha Baraza Kuu kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya kawaida, kama vile kuthibitisha jina la Katibu Mkuu, Manaibu Katibu Wakuu na wajumbe wa Kamati Kuu walioteuliwa na Mwenyekiti wa Chama.”
Mnyika pia alikanusha madai kwamba baadhi ya waliokuwepo kwenye kikao hicho hawakuwa wajumbe halali, akisema:
“Lilian Masiaga na Injinia Dk. Nyamatari Tengecha si wajumbe wa Baraza Kuu na hawapo kwenye orodha ya mahudhurio. Kwa hiyo, kuwepo au kutokuwepo kwao hakuwezi kuathiri akidi wala kubatilisha maamuzi yaliyofanyika.”
Aliongeza kuwa Mchome hakuhudhuria kikao hicho na kwamba:
“Inaelekea malalamiko yako yametokana na maneno ya kuambiwa ama ya kuhisi, lakini yasiyokuwa na ukweli au msingi wowote.”
Katika wito wake kwa wanachama, Mnyika alisisitiza umuhimu wa kutafuta ukweli kabla ya kusambaza taarifa zisizo sahihi:
“Ingependeza sana kama mwanachama na kiongozi wa chama kama ungetafuta ukweli wa jambo hili kwenye ofisi yangu kwanza kabla ya kuandika na kusambaza uzushi huu mitandaoni na kwenye vyombo vya habari na hivyo kuleta taharuki ya bure kwa wanachama na wananchi.”
Kwa sasa, CHADEMA imedhamiria kutetea nafasi na uhalali wa viongozi wake kupitia njia za kisheria, huku ikiwataka wanachama wake na Watanzania kwa ujumla kuendelea kuwa watulivu wakisubiri mwelekeo wa haki kupitia mahakama.
0 Comments:
Post a Comment