Msajili Atengua Uteuzi wa Viongozi Nane wa CHADEMA kwa Kukosa Akidi Halali



Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imetengua uteuzi wa viongozi wanane wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) waliothibitishwa na Baraza Kuu la chama hicho Januari 22, 2025, baada ya kubaini kuwa kikao kilichofanya uteuzi huo hakikufikia akidi halali ya wajumbe.


Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na tovuti ya Mwananchi Jumanne, Mei 13, 2025, uamuzi huo umefikiwa kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa na Lembrus Mchome, Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, aliyepinga uhalali wa kikao hicho kwa madai kuwa idadi ya wajumbe haikufikia kiwango kinachotakiwa.

Viongozi waliotenguliwa ni John Mnyika (Katibu Mkuu), Amani Golugwa (Naibu Katibu Mkuu Bara), Ally Ibrahim Juma (Naibu Katibu Mkuu Zanzibar), Godbless Lema, Rose Mayemba, Salma Kasanzu, Hafidh Ally Saleh na Dk. Rugemeleza Nshala ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa chama. Viongozi hao walikuwa wajumbe wa Kamati Kuu.

Ofisi ya Msajili imeielekeza CHADEMA kuitisha Baraza Kuu jipya lenye akidi halali kwa ajili ya kufanya uteuzi mpya wa viongozi hao kwa mujibu wa Katiba ya chama, Sheria ya Vyama vya Siasa na kanuni zake.

Akizungumzia suala hilo katika mafunzo ya viongozi wa BAWACHA na BAVICHA Kanda ya Kusini yaliyofanyika Machi 25, 2025, Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, alisema:
“Akidi ya kikao ilikuwa halali kwa kuwa kilihusu uteuzi wa kawaida, si mabadiliko ya katiba wala uchaguzi. Tulikuwa na zaidi ya asilimia 50 ya wajumbe, hiyo ni akidi ya kutosha kwa mujibu wa taratibu zetu.”

Hata hivyo, baada ya kuchambua malalamiko ya Mchome pamoja na majibu ya CHADEMA, Ofisi ya Msajili imekubaliana kwamba kikao hakikufikia akidi inayotakiwa, na hivyo uamuzi wake si halali.

Taarifa kutoka kwa chanzo cha ndani ya CHADEMA kilichozungumza na Mwananchi zinaeleza kuwa:
“Hii ni taarifa mbaya sana kwa chama. Inaweka chama kwenye hatari ya kisheria kama hakitatekeleza maelekezo ya msajili.” Chanzo hicho kimeongeza kuwa baadhi ya viongozi waliotenguliwa kwa sasa wako mikoani wakishiriki katika operesheni ya "No Reforms, No Election."

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa CHADEMA, Brenda Rupia, alieleza:
“Nimesikia kuhusu taarifa hizo, bado nazifuatilia. Chama kitapata taarifa rasmi mara tu zitakapothibitishwa.”

Kwa upande wake, Lembrus Mchome alisema Jumanne kuwa anatarajia kuzungumza na wanahabari Jumatano, Mei 14, 2025, kuhusu uamuzi wa Msajili kuhusiana na malalamiko aliyowasilisha, akisema:
“Siwezi kusema nimekubali au nimekataa kwa sasa. Nitazungumza rasmi kesho.”

Jitihada za Mwananchi kuwapata viongozi wa Ofisi ya Msajili, akiwemo Msajili Jaji Francis Mutungi na Naibu wake Sisty Nyahoza, hazikufanikiwa hadi kufikia wakati wa kuchapishwa kwa habari hiyo. Taratibu za kuwatafuta bado zinaendelea.

0 Comments:

Post a Comment