Waziri Silaa Azindua Kampeni ya “SITAPELIKI” Kupambana na Ulaghai Mtandaoni

 

Serikali, watoa huduma za simu na intaneti kushirikiana kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kujikinga na utapeli mtandaoni



Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, amezindua kampeni ya taifa ya "SITAPELIKI" iliyolenga kutoa elimu kwa umma kuhusu mbinu zinazotumiwa na matapeli mtandaoni na jinsi ya kujikinga na udanganyifu huo. 



Uzinduzi wa kampeni hiyo umefanyika leo Februari 20,2025 jijini Arusha na kuhudhuriwa na wadau umuhimu kutoka sekta ya mawasiliano na teknolojia ya habari, wakiwemo viongozi kutoka Wizara ya Mawasiliano, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Benki Kuu ya Tanzania (BOT), na makampuni ya simu.



"Leo hii, tupo katika mkutano huu wa kuzindua kampeni ya pamoja ya utoaji elimu kwa umma na kuwa na mpango mahususi wa kushughulikia masuala ya utapeli mtandaoni iitwayo 'SITAPELIKI.'


Kampeni hii inalenga katika kuongeza uelewa kuhusu mbinu zinazotumiwa na matapeli wa mtandaoni na kuwapa wananchi maarifa zaidi ya jinsi ya kujikinga dhidi ya majaribio mbalimbali ya ulaghai," alisema Waziri Silaa.

Katika hotuba yake, Waziri Silaa alieleza kuwa kampeni hii ni sehemu ya jitihada za serikali kushirikiana na watoa huduma za simu na intaneti kutoa elimu na kuongeza ufanisi katika kupambana na utapeli mtandaoni. 

Aliongeza kuwa utapeli huu unahujumu maendeleo ya nchi kwa kuwatia hofu watumiaji wa huduma za mtandao, na hivyo kudumaza juhudi za serikali za kuhamasisha matumizi ya mifumo ya kidijiti na kujenga uchumi wa kidijiti.

"Kampeni hii ya SITAPELIKI ina lengo la kutoa elimu kwa jamii pamoja na kuchukua hatua mahususi katika kushughulikia masuala ya utapeli mtandaoni," alisisitiza.

Kampeni hii pia inatarajiwa kuwawezesha wananchi kujua jinsi ya kulinda taarifa zao mtandaoni, kama vile nywila (neno la siri), na kujiepusha na viunganishi (links) visivyojulikana. Waziri Silaa alisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kuwa makini na maswala haya ya usalama mtandaoni.

"Linda taarifa zako kwa kutumia nywila thabiti na tofauti kwa kila akaunti, yenye mchanganyiko wa maneno, namba, alama na herufi kubwa na ndogo. Usifuate maelekezo na kutoa nywila (neno siri) au namba yako ya uthibitisho (OTP) kwa mtu yeyote," aliongeza.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa wananchi kuhakiki namba zao za simu kwa kutumia namba *106# ili kudhibiti wizi wa taarifa na kuongeza usalama. 


Alivipongeza pia vyombo vya habari kwa kushirikiana na serikali katika kusambaza elimu hii kwa wananchi.

"Tunahimiza kuhakiki namba zako za simu kupitia 106#. Bofya 106# kisha chagua kuona namba zilizo sajiliwa na kitambulisho chako cha NIDA. Iwapo utakuta namba usizo fahamu tafadhali fika kwenye duka la mtoa huduma wako ili waifute," alisisitiza Waziri Silaa.



Waziri alikumbusha kuwa watoa huduma wa mawasiliano ya simu wanapaswa kuwasiliana na wateja wao kupitia namba 100 pekee na si vinginevyo, akitoa wito kwa wananchi kutojibu simu za kutoka namba nyingine ambazo hazijulikani.

Katika kufafanua kuhusu ushirikiano wa taasisi za kifedha, Waziri Silaa alitolea mfano wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) ambayo inaendelea kushughulikia masuala ya usalama wa fedha mtandaoni, ikiwemo kuimarisha Dawati Maalumu la Malalamiko (Complaints Resolution Desk) na Kituo cha Kuitikia Majanga ya Kompyuta cha kisekta (TZ-FinCERT).


"Ninawapongeza Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kwa kuendelea kushughulikia masuala yote yanayohusu fedha katika mitandao ikiwa ni pamoja na kuimarishwa kwa Dawati Maalumu la Malalamiko (Complaints Resolution Desk) kwa ajili ya kutatua malalamiko ya wateja wa huduma za Kifedha," alisema.


Vilevile, Waziri Silaa alikishukuru Jeshi la Polisi Tanzania kwa juhudi za kukabiliana na wahalifu wa mtandaoni na kutoa rai kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuendelea kuchukua hatua madhubuti ili kupunguza au kuondoa kabisa tatizo la uhalifu mtandaoni.


"Ninatoa rai kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi kupitia Jeshi letu la Polisi kuendelea kuchukua hatua stahiki kwenye yale maeneo ambayo yanaripotiwa mara kwa mara kwa kuongoza katika viashiria vya Uhalifu mtandaoni," aliongeza.


Kwa upande wa malalamiko kutoka kwa watumiaji wa huduma za mawasiliano, Waziri Silaa alikumbusha wananchi kuwa wafuate utaratibu wa kuwasilisha malalamiko yao kwa watoa huduma kupitia namba 100, na kama hawatapata ufumbuzi, basi waendelee na malalamiko kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kupitia namba ya bila malipo 0800008272.


"Hivi karibuni, kumekuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya watumiaji wa huduma za mawasiliano. Tunawahimiza wananchi wafuate utaratibu wa kuwasilisha malalamiko yao kwa watoa huduma kupitia namba 100," alisema.

Waziri Silaa alisisitiza umuhimu wa kushirikiana na wadau wote ili kufanikisha kampeni hii na kuhakikisha kuwa elimu inafika kwa kila mtumiaji wa huduma za mawasiliano, hivyo kupunguza vitendo vya utapeli mtandaoni.


"Ni matumaini yangu kwamba baada ya kuzindua kampeni hii kila mdau ataenda kutekeleza kwa wakati mpango huu mahususi ambao utafanikisha lengo la kupeleka elimu na uelewa katika jamii juu ya kujikinga dhidi ya utapeli mtandaoni," alisistiza Waziri Silaa.


Uzinduzi wa kampeni ya “SITAPELIKI” unalenga kuongeza usalama wa mitandao na kuhakikisha kuwa wananchi wanatumia huduma za kidijiti kwa usalama zaidi, na hivyo kuchangia katika maendeleo ya uchumi wa kidijiti wa taifa.


Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Khamis Abdulla, amesema kikao kazi hicho kimejikita katika kutathmini utekelezaji wa Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali wa miaka 10, kuanzia 2024 hadi 2034.


Ameongeza kuwa mkakati huu utakuwa na nguzo sita muhimu, ambazo ni: kuwezesha miundombinu ya kidijitali, utawala na mazingira wezeshi, uelewa wa kidijitali na maendeleo ya ujuzi, utamaduni wa ubunifu wa kidijitali, teknolojia wezeshi na kukuza ushirikishwaji wa kidijitali na upatikanaji wa huduma za kifedha za kidijitali.


0 Comments:

Post a Comment