Serikali yatoa mwanga kuhusu changamoto za hisa za Vodacom na mwelekeo mpya wa sekta ya mawasiliano
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, amesema ni wakati muafaka kwa serikali kufanya mapitio ya sheria na mikakati ya uwekezaji katika sekta ya mawasiliano, ili kuhakikisha kuwa inawafaidi wananchi na kuwa na mazingira bora ya biashara kwa watoa huduma za simu na intaneti.
Kauli hiyo ameitoa leo Februari 20, 2025 jijini Arusha wakati akijibu maswali yaliyoulizwa kwenye majadiliano wakati wa uzinduzi wa kampeni ya "SITAPELIKI".
Waziri Silaa alieleza kuwa serikali ipo tayari kurejea kwenye meza ya mazungumzo na wadau wa sekta hiyo ili kutathmini hatua zilizochukuliwa awali na kurekebisha miongozo na sheria ili kuendana na mabadiliko ya soko na mazingira ya uwekezaji.
"Ni wakati muafaka wa sisi kukaa na kuangalia tulipofika na kutengeneza njia bora zaidi ya kampuni hizi kujiendesha hasa tukiweka mazingatio kwenye miongozo na vision aliyonayo Rais Samia Suluhu Hassan.
Rais Samia amefanya kazi kubwa kukuza mazingira ya uwekezaji, sisi tunaomsaidia hatuna budi kuangalia namna ya kusaidia utekelezaji wa mikakati hii muhimu kwa manufaa ya Watanzania wote," alisema Waziri Silaa.
Waziri Silaa alikiri kuwa baadhi ya hatua zilizochukuliwa katika kipindi cha nyuma, ikiwemo sheria iliyolazimisha Vodacom kujisajili kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) mwaka 2017, hazikuzalisha matokeo yaliyotarajiwa.
Alisema kuwa wazo la serikali kuhamasisha wananchi kununua hisa za Vodacom lilileta matumaini makubwa lakini utekelezaji wake haukuwa mzuri, na hivyo kuleta changamoto kwa watanzania waliowekeza.
"Mimi nadhani njia bora zaidi ya kukuza sekta yoyote kwenye uchumi huu wa soko ni kuacha sekta zitawaliwe na nguvu ya soko.
Kama serikali, tukianza kutengeneza shuruti kwenye baadhi ya mambo, matokeo yake ndio haya unayosema. Sina tathmini sahihi, lakini ndio hiki ulichokisema," alisema.
Aidha, Waziri Silaa alisema kuwa ni muhimu serikali kufanya mapitio ya sheria zilizopitishwa na kurekebisha mikakati ya sekta hiyo kwa manufaa ya pande zote, akiongeza kuwa hakuna mfumo wa sheria unaoweza kuwa kamili kila wakati.
Aliweka wazi kuwa kupitia vikao vya wadau, serikali itachukua hatua za kuboresha mazingira ya biashara na kuhakikisha uwekezaji katika sekta ya mawasiliano unakua.
"Lakini ambacho naweza kusema ni kwamba ni wakati wa kufanya mapitio na kujua tulipo, na kutengeneza utaratibu bora zaidi kwa ajili ya sekta hii," aliongeza.
Katika majadiliano hayo, mwandishi wa habari mkongwe nchini, Absalom Kibanda, aliuliza maswali kadhaa muhimu kuhusu hatima ya wawekezaji wa Vodacom baada ya serikali kuhamasisha wananchi kununua hisa za kampuni hiyo kupitia sheria zilizowekwa mwaka 2017.
Kibanda alikosoa hatua ya serikali ya kuhamasisha wananchi kuwekeza kwenye kampuni za simu kabla ya kuandaa mazingira rafiki ya uwekezaji.
"Serikali imechukua hatua gani ili kuwasaidia wanahisa waliohamasishwa na serikali mwaka 2017 kununua hisa za Vodacom ambao hadi leo hawajui hatima ya uwekezaji wao katika hiyo kampuni?" alihoji Kibanda.
Alitilia mkazo pia changamoto zinazojitokeza kutokana na kushuka kwa thamani ya hisa za Vodacom, akisema kuwa wananchi wengi ambao walijitokeza kuwekeza wameshindwa kuelewa jinsi gani thamani ya hisa zao ilivyoshuka kutoka TZS 850 hadi TZS 740.
"Je, serikali haioni kwamba uamuzi ule wa kuilazimisha Vodacom kusajiliwa katika soko la hisa kabla ya kuandaliwa kwa mazingira rafiki ndiko ambako kumesababisha sintofahamu iliyopo?" alihoji Kibanda.
Alitahadharisha kuhusu hatari ya kuwa na hali hii ambayo inaweza kuleta hasara kwa wananchi, akizungumzia kuhusu uwekezaji wa umma ambao ulifanywa bila ya mazingira mazuri ya biashara, na kuuliza serikali itachukua hatua gani sasa ili kuwanusuru wananchi walioshawishiwa kuwekeza.
"Je, serikali itachukua hatua gani sasa ili kuwanusuru na hasara kubwa Watanzania walioshawishiwa na serikali kuwekeza katika kampuni ya Vodacom?"
Kibanda alihoji pia iwapo serikali imejifunza kutokana na makosa ya awali, hasa katika kulazimisha kampuni za simu kujiingiza sokoni kabla ya kuwa na mazingira ya soko bora.
"Je, serikali imejifunza nini kutokana na kosa hilo la kuzilazimisha kampuni za simu kuchukua hatua za kiuwekezaji kama ilivyoifanyia Vodacom mwaka 2017 kwa kujisajili DSE huku ikijua kwamba hakukuwa na mazingira mwafaka ya kufanya hivyo?" alihoji Kibanda.
Vodacom na Hisa Zake
Vodacom Tanzania ilikuwa ya kwanza kutekeleza sheria ya EPOCA ya 2010 na Sheria ya Fedha ya 2016 kwa kuuza hisa 25% kwa umma kupitia Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) mwaka 2017.
Hisa hizo ziliuzwa kwa shilingi 850, na serikali ilijivunia hatua hiyo ya kuwapa Watanzania fursa ya kuwekeza katika kampuni kubwa ya mawasiliano.
Hata hivyo, thamani ya hisa hizo imeshuka kwa kiasi kikubwa, ambapo kwa mujibu wa hesabu za Vodacom PLC zinazoishia mwezi Machi 2024 hisa moja inauzwa kwa shilingi 740, jambo ambalo limetokea kama changamoto kubwa kwa wawekezaji wa Vodacom, hasa wale walionunua hisa hizo kwa bei ya juu.
Hali ya soko inavyoendelea kuonyesha kushuka kwa thamani ya hisa kwa shilingi 110 kumebainisha udhaifu wa utekelezaji wa mpango huu.
Waziri Silaa alisisitiza kuwa serikali itachukua hatua zinazofaa kuhakikisha maslahi ya Watanzania yaliyowekeza katika kampuni hiyo yanahifadhiwa kwa kuangalia namna ya kuboresha utaratibu wa uwekezaji na usajili wa kampuni za simu nchini.
"Sheria hatuzitungi sisi kutu control. Sheria tunazitunga ku regulate na kupeleka mambo yetu mbele," alisema Waziri Silaa, akisisitiza umuhimu wa kuboresha sheria na miongozo ili sekta ya mawasiliano iweze kutoa matokeo bora kwa Watanzania wote.
Kwa ujumla, Waziri Silaa alikiri kuwa ingawa hatua zilizochukuliwa awali zilikuwa na nia nzuri, ni muhimu sasa kurekebisha mikakati ili kuhakikisha kuwa sekta ya mawasiliano inakuwa imara na inatoa fursa kwa kila mtu.

0 Comments:
Post a Comment