Ongezeko la Watalii Na Maendeleo Katika Sekta ya Maliasili Na Utalii

 


Sekta ya utalii nchini Tanzania imeendelea kukua kwa kasi, huku idadi ya watalii ikifikia milioni 5.3 na mapato yatokanayo na utalii yakifikia dola za Kimarekani bilioni 3.6. 



Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Pindi Chana, amesema kuwa mafanikio haya yanatokana na juhudi mbalimbali za serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ikiwemo uboreshaji wa miundombinu na utangazaji wa vivutio vya utalii kimataifa.


Dkt. Pindi Chana amesema,

"Tumefanikiwa kuongeza idadi ya watalii mpaka sasa; tumefikia watalii milioni 5.3 na mapato yatokanayo na utalii yamefikia dola za kimarekani bilioni 3.6. Hii ni ishara kuwa sekta ya utalii inakua kwa kasi na inachangia zaidi katika uchumi wa nchi."


Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli zake kwa kipindi cha Februari 2024 hadi Januari 2025, huku likiiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kufanya maboresho zaidi katika sekta ya maliasili na utalii ili kuimarisha mchango wake katika uchumi wa taifa.



Katika kikao cha 9 cha Mkutano wa 18 wa Bunge, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Timotheo Mnzava, aliielekeza Wizara ya Maliasili na Utalii kuboresha utaratibu wa makusanyo ya mapato katika taasisi za uhifadhi ili kurahisisha shughuli za uhifadhi na ukarabati wa miundombinu katika maeneo ya hifadhi.


Timotheo Mnzava amesema,

"Ni muhimu kuboresha utaratibu wa makusanyo ya mapato katika taasisi za uhifadhi ili kurahisisha shughuli za uhifadhi, ikiwa ni pamoja na ukarabati wa miundombinu ndani ya maeneo ya hifadhi. Vilevile, tunawahimiza wakurugenzi wa taasisi hizo kugundua mazao mapya ya utalii na kutumia njia za kidijitali kutangaza vivutio vya utalii nchini."

 

Aidha, Mnzava ameongeza kuwa Wizara inapaswa kufanya tathmini ya hoteli na lodges za serikali zilizobinafsishwa kwa wawekezaji ili kuhakikisha usimamizi bora wa mapato na uendeshaji wake.


Dkt. Pindi Chana ameweka wazi kuwa serikali itaendelea kuboresha miundombinu na huduma za malazi katika maeneo ya hifadhi ili kuongeza ubora wa huduma kwa watalii. 


Amesema kuwa tayari Shirika la UNESCO limetoa kibali cha kuridhia ujenzi wa barabara ya tabaka gumu kutoka Nabi hadi Fort Ikoma katika eneo la Ngorongoro.


"Serikali inaendelea kuchukua hatua kuhakikisha sekta ya utalii inazidi kukua. Tayari tumepata kibali cha UNESCO kwa ujenzi wa barabara muhimu kutoka Nabi hadi Fort Ikoma, ambayo itarahisisha usafiri ndani ya eneo la hifadhi," amesema Dkt. Pindi Chana.

 

Kuhusu maandalizi ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wa dunia wa Ufugaji Nyuki (APIMONDIA) 2027, Dkt. Pindi Chana amefafanua kuwa tayari eneo lenye ukubwa wa ekari 48 limepatikana kwa ajili ya mkutano huo, na mchakato wa kumpata mkandarasi kwa ajili ya ujenzi unaendelea.


Hatua hizi zote zinadhihirisha juhudi za Bunge na serikali katika kuboresha na kuendeleza sekta ya maliasili na utalii, ikiweka msingi imara wa maendeleo endelevu katika sekta hii muhimu kwa uchumi wa taifa.

0 Comments:

Post a Comment