SADC na EAC Zatafuta Suluhu ya Kudumu kwa Mgogoro wa DRC

 


Mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamekutana leo jijini Dar es Salaam, Tanzania, kujadili suluhu ya kudumu kwa mgogoro unaoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).


Kikao hicho kinatangulia mkutano wa marais wa jumuiya hizo utakaofanyika hapo kesho kwa lengo la kuimarisha juhudi za kurejesha amani katika eneo hilo.


Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Musalia Mudavadi, ambaye ni mwenyekiti mwenza wa mkutano huo, amesema kuwa ni wakati mwafaka kwa SADC na EAC kushirikiana ili kuwasaidia wananchi wa DRC.


"Hali hii inahitaji tuchukue hatua za haraka, kwa pamoja, na kwa njia endelevu," amesema Mudavadi.


Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, ameonyesha wasiwasi wake kuhusu hali ya usalama nchini DRC, akisema kuwa mgogoro huo unaathiri vibaya hali ya kibinadamu na kutishia usalama wa ukanda mzima.


"Tunakutana sote hapa, tukiwa na mioyo ya kupata suluhu ya kudumu," amesema Balozi Kombo.


Mgogoro huo umekithiri zaidi baada ya waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda kuteka mji wa Goma na kukabiliana vikali na majeshi ya serikali ya DRC.


Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, karibu watu 3,000 wamefariki kutokana na makabiliano hayo, huku hali ya kibinadamu ikiendelea kuzorota.


Mkutano wa marais wa SADC na EAC unaotarajiwa kufanyika kesho unalenga kuweka mikakati madhubuti ya kurejesha amani na kuleta utulivu mashariki mwa DRC.


0 Comments:

Post a Comment