Serikali Kuboresha Tozo Za Wachimbaji Wadogo wa Dhahabu

 


Serikali, kupitia Wizara ya Madini, inaendelea na juhudi za kupunguza mzigo wa tozo kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu nchini. 


Hatua hii inalenga kufanya mapitio ya ada na ushuru mbalimbali unaotozwa katika mnyororo wa uchimbaji na uchenjuaji wa madini, huku ikizingatia maslahi ya wachimbaji wadogo na kukuza sekta ya madini.



Wakati wa mjadala uliofanyika Bungeni tarehe 7 Februari 2025, Waziri wa Madini Anthony Mavunde alijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Jimbo la Busanda Tumaini Magessa, ambaye alitaka kujua ni lini serikali itapitia upya tozo zilizopo kwenye mnyororo wa uchimbaji na uchenjuaji wa dhahabu. Anthony Mavunde alisema,

"Katika kutatua changamoto hizi, Wizara iliitisha kikao kilichofanyika mwezi Agosti 2024 Mkoani Singida, kilichoshirikisha Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Wizara ya Fedha, Tume ya Madini, STAMICO, pamoja na Halmashauri za Wilaya za Ikungi, Chunya, Kahama, Msalala, Meatu, Shinyanga, Mtama na Lindi, pamoja na FEMATA na TAWOMA. Rasimu ya Mapendekezo ya Maboresho tayari imeshaandaliwa na ipo katika hatua ya kufanyiwa mapitio na tathmini. Matokeo ya tathmini hiyo yatatusaidia kupanga tozo rafiki kwa wachimbaji wadogo."

Aidha, Anthony Mavunde aliendelea,

"Serikali inaendelea na maboresho makubwa ya mfumo wa kodi kupitia Tume ya Maboresho ya Kodi iliyoanzishwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Tume hiyo inatarajiwa kutoa mapendekezo yatakayosaidia kupunguza changamoto za kikodi zinazowakabili wachimbaji wadogo wa dhahabu na sekta ya madini kwa ujumla."

Hatua hizi zinadhihirisha dhamira ya serikali ya kuboresha mazingira ya uchimbaji mdogo wa madini na kukuza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa nchi.

0 Comments:

Post a Comment