MSUGUANO MKALI NDANI YA TLP, MSAJILI WA VYAMA AWAPA SIKU SABA KUJIELEZA

 

Mambo bado hayajatulia ndani ya Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), ambapo Msajili wa Vyama vya Siasa nchini amewapa muda wa siku saba viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi wa Februari 2, 2025, kujieleza kuhusu madai ya ukiukwaji wa Katiba ya chama hicho.

Hatua hiyo imekuja baada ya wanachama wa TLP kuwasilisha malalamiko kwa Msajili, wakipinga uchaguzi uliofanyika katika hoteli ya Mrina, Manzese, Dar es Salaam, wakidai kuwa uongozi uliopo madarakani haupo kihalali.

Wanachama wadai uchaguzi ulikuwa batili



Akizungumza na wanahabari jijini Arusha, Katibu Mwenezi wa TLP Taifa, Geoffrey Steven, alisema: "Wanachama wa chama chetu wameandika barua kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kupinga uchaguzi huo kwa sababu viongozi waliopo hawakuchaguliwa na wanachama halali bali na watu wa kuokoteza mitaani waliovishwa sare za chama."

Ameeleza kuwa chama kina wanachama katika mikoa yote Tanzania Bara na Visiwani, na kwamba mkutano mkuu wa uchaguzi ulipaswa kushirikisha wajumbe 185 waliopo kwenye rejista rasmi ya chama.

"Hata hivyo, wajumbe wengi wa mkutano mkuu hawakuhudhuria kwa sababu taarifa ya mkutano ilitolewa ndani ya siku mbili tu, jambo ambalo ni kinyume na katiba ya chama na kanuni za uchaguzi," alisema Geoffrey.



Kwa mujibu wa Katibu wa TLP Mkoa wa Arusha, Kinanzaro Mwanga, ambaye pia alikuwa mgombea wa Uenyekiti Taifa, uchaguzi huo haukufuata taratibu za chama.

"Katiba ya TLP toleo la mwaka 2009 inaelekeza kuwa uchaguzi uanzie ngazi za chini na utamalizika ngazi ya taifa, lakini cha ajabu uchaguzi wa taifa umefanyika bila kufanyika kwa chaguzi ngazi za chini," alisema Mwanga.

Ameongeza kuwa katika nafasi ya Uenyekiti Taifa, kulikuwa na wagombea watano waliopitishwa na Halmashauri Kuu ya Taifa Februari 5, 2024, lakini baadhi yao hawakupata taarifa ya mkutano na hivyo hawakuhudhuria.


Wagombea waliopitishwa walikuwa Richard Lyimo (aliyekuwa Katibu Mkuu Taifa), Abu Chagawa, Livan Maganza, Stanley Ruyamgabo na Kinanzaro Mwanga.


"Wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi walipaswa kuwa Wenyeviti wa mikoa, Makatibu wa mikoa na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa kutoka kila mkoa. Jumla yao ni 185, lakini zaidi ya robo tatu hawakuhudhuria kwa sababu hawakutaarifiwa," alisema Mwanga.

Msajili wa Vyama vya Siasa ataka ufafanuzi



Kutokana na malalamiko hayo, Msajili wa Vyama vya Siasa ametoa muda wa siku saba kwa uongozi uliopo madarakani kujieleza kuhusu tuhuma hizo za ukiukwaji wa katiba na taratibu za uchaguzi.

Wanachama wa TLP wamesema kuwa endapo Msajili wa Vyama vya Siasa hatachukua hatua za kufuta uchaguzi huo, watachukua hatua zaidi, ikiwemo kufungua kesi mahakamani ili kutaka uongozi huo kutotambuliwa rasmi.

"Tunamuomba Msajili aingilie kati ili uchaguzi huo ufutwe na mchakato uanze upya kwa kufuata katiba ya chama," alisema Kinanzaro Mwanga.

Kwa sasa, hali ndani ya TLP inaendelea kuwa na sintofahamu, huku wanachama wengi wakisubiri majibu kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusu hatua zitakazochukuliwa ili kutatua mgogoro huo.

0 Comments:

Post a Comment