Bilionea Elon Musk, mkuu wa Idara ya Ufanisi wa Serikali (Doge), alitangaza kupitia mtandao wa X kwamba wafanyakazi wa serikali ya Marekani "watapokea barua pepe hivi karibuni wakiomba kuelewa walichofanya wiki iliyopita." Musk aliandika kwamba "Kukosa kujibu kutachukuliwa kama kujiuzulu."
Hatua hii ni sehemu ya juhudi za serikali ya Rais Donald Trump kupunguza matumizi ya serikali kwa njia ya kupunguza wafanyakazi na ufadhili.
Barua pepe hiyo iliwasili Jumamosi alasiri kwa wafanyakazi wa serikali, ikiwauliza waorodheshe mafanikio yao ya wiki iliyopita au wajiuzulu. Ujumbe wa barua pepe ulijumuisha maswali ya wazi: "Ulifanya nini wiki iliyopita?" kutoka kwa mtumaji aliyeorodheshwa kama HR.
Ofisi ya Usimamizi wa Wafanyikazi (OPM), wakala wa serikali ya shirikisho la rasilimali watu, ilithibitisha kuwa barua pepe hiyo ilikuwa ya kweli kupitia taarifa kwa CBS, mshirika wa habari wa BBC wa Marekani.
OPM ilisema, "Kama sehemu ya dhamira ya utawala wa Trump kwa wafanyakazi wenye ufanisi na wanaowajibika, OPM inawaomba wafanyakazi watoe muhtasari mfupi wa walichofanya wiki iliyopita kufikia mwisho wa Jumatatu, kumjulisha meneja wao."
Barua pepe hiyo ilifuatia hotuba ya Rais Trump katika Mkutano wa Kisiasa wa Kihafidhina (CPAC). Wafanyakazi walitakiwa kuelezea mafanikio yao ya wiki iliyopita kwa kifupi, bila kufichua habari za siri, kabla ya saa sita usiku Jumatatu.

0 Comments:
Post a Comment