Rais Tshisekedi Atangaza Kutohudhuria Mkutano wa EAC kuhusu Mgogoro wa Goma

 




Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Félix Tshisekedi, amethibitisha kuwa hatahudhuria mkutano wa dharura wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ulioitishwa na Rais William Ruto wa Kenya, kuzungumzia mgogoro wa kiusalama unaoendelea katika jimbo la Kivu Kaskazini, mashariki mwa DRC. 


Mkutano huo ulifanyika tarehe 29 Januari 2025, kwa njia ya mtandao na ulikusudiwa kujadili mzozo unaoendelea mjini Goma, ambapo hali ya usalama imezidi kuwa mbaya.


"Rais Félix Tshisekedi anafuatilia kwa karibu matukio yanayoendelea mashariki mwa nchi. 


Hata hivyo, hana mipango ya kuhudhuria mkutano ulioitishwa na Rais William Ruto," alithibitisha Giscard Kusema, Naibu Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano katika ofisi ya Rais, alipokuwa akizungumza na gazeti la Actualite.cd. 


Kusema aliongeza kuwa Tshisekedi atatoa hotuba jioni kupitia matangazo ya moja kwa moja kutoka ofisi zake.


Rais William Ruto, ambaye pia ni Mwenyekiti wa EAC, aliitisha mkutano huo ili kuzungumzia mzozo unaozidi kushika kasi katika mji wa Goma, ambao umesababisha madhara makubwa kwa raia na usalama wa eneo zima. 


"Nimezungumza na Rais Tshisekedi na Rais Kagame wa Rwanda ili kujitahidi kutuliza hali katika eneo hili," alisema Ruto alipozungumza na vyombo vya habari.

Rwanda inashutumiwa na DRC kwa kuunga mkono waasi wa kundi la M23, ambao wamekuwa wakitekeleza mashambulizi katika mji wa Goma na kuhusishwa na tishio kubwa la usalama katika mkoa wa Kivu Kaskazini. 


Hata hivyo, Rwanda inajitetea kwa kusema kuwa inajihami kutokana na usalama wake kutishiwa na waasi wa FDLR, wanaoendesha mapigano katika mashariki mwa DRC.

Wakati wa mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Marekani ilisisitiza kuwa hatua lazima zichukuliwe ili kuzuia vikosi vya Rwanda na waasi wa M23 kuendelea kuingia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. 


Kaimu Balozi wa Marekani kwa Umoja wa Mataifa, Dorothy Shea, alisisitiza kuwa "Tunataka kusitisha na kumaliza mapigano haraka iwezekanavyo. Rwanda lazima iondoe wanajeshi wake DRC. Rwanda na DRC lazima warudi kwenye meza ya mazungumzo na kushirikiana katika kupatikana kwa suluhisho endelevu na la amani."


Waasi wa M23, wanaoungwa mkono na Rwanda, waliandamana hadi Goma, mji mkubwa zaidi mashariki mwa DRC, na kuleta hali ya wasiwasi mkubwa. DRC ililaumu Rwanda kwa kutuma wanajeshi wake mpakani, huku Rwanda ikisema mapigano karibu na mpaka yanatishia usalama wake.


Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC, Therese Kayikwamba Wagner, alitoa wito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuweka vikwazo dhidi ya viongozi wa kijeshi na kisiasa wa Rwanda, ikiwemo vikwazo vya silaha, marufuku ya ununuzi wa maliasili za Rwanda na kuzuiwa kwa wanajeshi wa Rwanda kutoka kwa ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa.


Katika muktadha huu wa mzozo, viongozi wa DRC wamehamasisha kampeni za "usajili wa kizalendo" kwa vijana kujiandikisha katika jeshi ili kukabiliana na waasi. 


Waziri wa Mipango, Guy Loando Mboyo, alizindua kampeni ya "Tuchukue Hatua Kwa Ajili ya Nchi Yetu, Tunakataa Vita," kwa lengo la kuwashawishi vijana kujiunga na jeshi la nchi.


Hata hivyo, mji wa Goma umeathiriwa sana na mashambulizi, huku makombora yakirushwa juu ya nyumba za raia. Myriam Favier, msemaji wa Msalaba Mwekundu (ICRC), alielezea hali ya kiusalama kuwa ni mbaya sana, akisema "Ni eneo lenye watu wengi ... waathiriwa ni wengi upande wa raia."


Licha ya machafuko hayo, maduka kadhaa katika mkoa wa Nyiragongo, kaskazini mwa Goma, yalifunguliwa kwa saa chache, kutoa fursa kwa watu kununua chakula. 


Hata hivyo, Bi Favier alisema, "Hakujakuwa na umeme, ambayo inamaanisha kuwa hakuna maji katika jiji pia," jambo linaloongeza mzigo kwa wananchi waliokumbwa na maafa hayo.

0 Comments:

Post a Comment