Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, amezindua rasmi teknolojia ya kuondoa uvimbe mwilini bila upasuaji inayojulikana kama High-Intensity Focused Ultrasound (HIFU) katika Hospitali ya Kairuki, Dar es Salaam. Uzinduzi huu ni wa kwanza kufanyika katika Afrika Mashariki na Kati.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Agosti 27, 2025, Dkt. Biteko amesema huduma hiyo ni hatua kubwa kwa taifa na inadhihirisha kasi ya maendeleo katika sekta ya afya nchini.
"Ni teknolojia ya kipekee ambayo itarahisisha maisha ya Watanzania wengi na pia kupunguza gharama za matibabu nje ya nchi. Tanzania sasa ni miongoni mwa mataifa manne barani Afrika yanayotoa huduma hii, pamoja na Misri, Nigeria na Afrika Kusini," amesema Dkt. Biteko.
Aidha, ameipongeza Hospitali ya Kairuki kwa kutoa punguzo la asilimia 50 kwa wagonjwa 50 wa kwanza watakaopata huduma hiyo kwa mwezi wa mwanzo.
"Hii ni ishara ya upendo na kujali, lakini pia ni kuunga mkono juhudi za Serikali ya kutoa huduma nafuu kwa wananchi," amesema.
Ameeleza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kuimarisha huduma za afya, huku akiwaasa watendaji wa Wizara ya Afya kuwa na moyo wa kujifunza.
"Watendaji wa wizara wasiogope kujifunza pale sekta binafsi inapofanya vizuri. Lengo letu sote ni moja — huduma bora kwa wananchi," amesisitiza Dkt. Biteko.
Ameeleza kuwa uwekezaji wa teknolojia ya HIFU umegharimu shilingi bilioni 12 na milioni 300, na hadi sasa wagonjwa 303 wamepatiwa huduma ya uchunguzi huku 298 wakipata matibabu.
Amefafanua kuwa HIFU inatibu uvimbe mbalimbali ukiwemo wa saratani na usio wa saratani katika maeneo kama matiti, kongosho, kizazi na tezi dume, huku faida zake zikiwa ni pamoja na kutoacha kovu, mgonjwa kutopasuliwa, kupona haraka na kupunguza gharama za matibabu nje ya nchi.
Dkt. Kaganda ameongeza kuwa huduma hiyo pia husaidia kuboresha matokeo ya dawa za saratani, kupunguza kasi ya ukuaji wa saratani na kupunguza maumivu kwa wagonjwa.
Aidha, ameeleza kuwa Kairuki sasa ina Idara ya Huduma za Dharura yenye uwezo wa kuhudumia wagonjwa zaidi ya 9,000 kwa mwaka, ikiwa ni sehemu ya kujiandaa kutoa huduma bora kwa changamoto za afya za dharura.







0 Comments:
Post a Comment